Iran yakadhibisha madai ya Ufaransa kuhusu miradi yake ya anga za mbali
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa vikali madai ya uingiliaji wa mambo ya ndani ya taifa hili yaliyotolewa na Ufaransa kuhusu miradi ya anga za mbali ya Tehran.
Sayyid Abbas Mousavi amekabidhibisha kauli ya serikali ya Ufaransa kuhusu hatua ya hivi karibuni ya Iran ya kurusha satalaiti katika anga za mbali akisisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ina kila haki ya kupanua na kuboresha teknolojia yake ya anga za mbali.
Siku ya Jumatatu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa ilitoa taarifa eti ya kukosoa hatua ya Iran ya kurusha katika anga za mbali satalaiti yake ya 'Zafar' ikidai kuwa hatua hiyo inakiuka wajibu wa kimataifa wa Iran na Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Hata hivyo Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali matamshi hayo ya upotoshaji ya Paris na kueleza bayana kuwa, mradi wa makombora ya kujilinda wa Iran hauna mfungamanao wowote na azimio hilo la Baraza la Usalama la UN, kwa kuwa makombora ya Iran hayawezi kubeba vichwa vya silaha za nyuklia.
Siku chache zilizopita, Msemaji wa Shirika la Anga za Mbali la Iran (ISA) alisema, satalaiti ya Zafar iliyoundwa na wataalamu wa ndani imerushwa angani kwa mafanikio kwa kutumia roketi la kubebea satalaiti la Simorgh, ijapokuwa haikuweza kufika kwenye mzingo iliopangiwa.
Sayyid Ahmad Hosseini alisisitiza kwamba, taarifa zilizokusanywa katika kurusha angani satalaiti hiyo zitatumika kwa ajili ya kuboresha zaidi majaribio yajayo.