Wanafunzi wa Iran walaani mauaji ya Waislamu nchini India
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i59656-wanafunzi_wa_iran_walaani_mauaji_ya_waislamu_nchini_india
Vyama vya Kiislamu vya Wanafunzi wa Iran vimelaani vikali mauaji na hujuma za kinyama wanazofanyiwa Waislamu nchini India.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Mar 10, 2020 04:49 UTC
  • Wanafunzi wa Iran walaani mauaji ya Waislamu nchini India

Vyama vya Kiislamu vya Wanafunzi wa Iran vimelaani vikali mauaji na hujuma za kinyama wanazofanyiwa Waislamu nchini India.

Taarifa ya wanafunzi hao Waislamu wa Kiirani imesema kuwa, "Waislamu nchini India wanaendelea kushambuliwa na kukandamizwa kwa kutumia visingizio mbalimbali, jambo ambalo linawatia wasi wasi Waislamu wenzao kote duniani."

Vyama hivyo vya wanafunzi wa Iran vimeitaka Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran na taasisi nyingine husika hapa nchini kuikumbusha serikali ya New Delhi kuwa njia pekee ya kutatua mgogoro uliopo ni kufuata sheria na sio kuchukua hatua zisizo za ubinadamu.

Siku chache zilizopita pia, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliitahadharisha serikali ya India dhidi ya kuendelea kutekeleza mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo na kusisitiza kuwa, ukandamizaji unaoendelea kufanyiwa Waislamu katika nchi hiyo ya kusini mwa Asia utapelekea serikali ya New Delhi itengwe katika ulimwengu wa Kiislamu. 

 

Wahindu wenye misimamo mikali wakishambulia na kuchoma moto misikiti New Delhi

Aidha Tume ya Haki za Binadamu ya Vyombo vya Mahakama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani ukatili huo dhidi ya Waislamu na kuitaka serikali ya nchi hiyo ihakikishe haki za kiutu na kiraia za Waislamu hao zinalindwa.

Baada ya  Bunge la India mnamo Disemba 11, 2019 kupitisha marekebisho ya sheria ya uraia inayowabagua Waislamu, Waislamu na wasio Waislamu nchini India wamekuwa wakiandamana kupinga sheria hiyo ya tata hususan mjini New Delhi ambapo makumi ya Waislamu wameuawa na maafisa usalama wakishirikiana na Wahindu wenye misimamo mikali.