Iran yaitaka India kufuta sheria inayowabagua Waislamu
Mjumbe mmoja wa Baraza la Kulinda Katiba la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemwandikia barua Mkuu wa Mahakama Kuu ya India na kumtaka atumie ushawishi wake kufuta sheria mpya ya uraia inayowakandamiza Waislamu.
Shirika la habari la IRNA limemnukuu Hadi Tahan Nazif, mjumbe wa masuala ya kisheria wa Baraza la Kulinda Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akisema katika barua yake hiyo kwa Sharad Arvind Bobde, Mkuu wa Mahakama Kuu ya India kwamba habari zinazoripotiwa duniani hivi sasa kutoka India zinaonesha kuwa, kuna ukandamizaji na dhulma inayofanywa dhidi ya haki za kimsingi kabisa za kuishi za watu wa tabaka fulani.
Amesema ni jambo lisilo na shaka kwamba serikali ya India inapaswa kuchukua hatua zinazotakiwa za kuiepusha nchi hiyo kutumbukia kwenye vita vya kidini. Amefafanua zaidi kwa kusema, taswira waliyo nayo walimwengu kuhusu India si kitu kingine isipokuwa amani na kuishi pamoja kwa salama watu wa dini na madhehebu zote.
Mjumbe huyo wa Baraza la Kulinda Katiba la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vile vile amesema katika barua hiyo kwamba, inavyoonekana ni kuwa sheria ya uraia iliyopasishwa na bunge la India mwezi Disemba 2019 imejaa ubaguzi dhidi ya Waislamu ikiwemo haki yao ya kimsingi kabisa ya uraia.
Kwa mujibu wa sheria hiyo mpya ya uraia huko India, wakimbizi wa nchi za Bangladesh, Afghanistan na Pakistan waishio nchini India ambao hawana hati rasmi tangu kabla ya mwaka 2015 wanaweza kupata uraia wa India, isipokuwa Waislamu.
Wakati huo huo Wahindu na Mabaniani wenye misimamo mikali wamevamia maeneo ya Waislamu, misikiti na maeneo ya ibada huko kaskazini na mashariki mwa New Delhi na kuchoma moto, kuvunja maeneo hayo na kuwaua kikatili Waislamu.