Iran yatuma zana za kivita katika mpaka wa magharibi mwa nchi
(last modified Fri, 06 Nov 2020 10:39:18 GMT )
Nov 06, 2020 10:39 UTC
  • Iran yatuma zana za kivita  katika mpaka wa magharibi mwa nchi

Jeshi la nchi kavu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limetuma zana za kivita na wanajeshi katika ukanda wa mpaka wa Iran na Armenia na Jamhuri ya Azerbaijan.

Brigedia Jenerali Ali Hajloui, Kamanda wa Ukanda wa Kaskazini Magharibi wa Jeshi la Nchi Kavu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametangaza leo Ijumaa kuwa, jeshi liko tayari kulinda mpaka wa magharibi mwa nchi mkabala wa tishio lolote lile la adui. Amesema jeshi linalipa kipaumbele suala la utulivu wa wananchi wanaoishi katika maeneo ya mpakani.

Amongeza kuwa: "Kwa kuzingatia mapigano ya hivi karibuni baina ya Jamhuri ya Azerbaijan na Armenia, Jeshi la Nchi Kavu la Iran limepewa jukumu la kulinda eneo la kaskazini magharibi mwa nchi na kukabiliana na tishio lolote lile.

Zana za kivita za Jeshi la Iran zikiwa zinasafirishwa kuelekea magharibi mwa nchi

Maeneo ya mpakani katika mkoa wa Azerbaijan mashariki mwa Iran yanapakana na Jamhuri ya Azerbaijan na Armenia na hivi sasa nchi hizo mbili zinaendelea kupigania eneo linalozozaniwa la Nagorno Karabakh.

Tokea mgogoro wa Nagorno Karabakh uanze hadi sasa mamia ya maroketi ya pande mbili hasimu yamekuwa yakianguka katika eneo la Khoda Afarin ambalo lina mpaka wa kilomita 135 na nchi mbili zinazozozana.

 

 

Tags