Rouhani: Hatima ya Trump haitakuwa bora kuliko ya dikteta Saddam
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hatima ya Rais anayeondoka wa Marekani, Donald Trump haitakuwa bora kuliko ya dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein.
Rais Hassan Rouhani amesema hayo leo katika mkutano wa Baraza la Mawaziri hapa Tehran na kuongeza kuwa, "tumekuwa viumbe viwili wendawazimu katika historia ambao walianzisha vita dhidi ya ya taifa la Iran; mmoja alikuwa Saddam na mwingine ni Trump. Saddam alianzisha vita vya kijeshi dhidi yetu, na Trump akaanzisha vita vya kiuchumi."
Ameashiria kuhusu vita vya kichokozi vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran na kubainisha kuwa: Tuliungana katika vita hivyo na tukamshinda Saddam Aidha tulishuhudia siku ambayo mwendawazimu huyo aliponyongwa.
Dakta Rouhani ameeleza bayana kuwa, muqawama wa wananchi wa Iran dhidi ya vikwazo vya kiuchumi umepelekea kusambaratika ndoto za walioliwekea taifa hili mashinikizo hayo.
Rais wa Iran amebainisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imeipigisha mweleka Marekani katika uga wa kimataifa na kuongeza kuwa: (Wamarekani) walitengwa. Kila mara walipowasilisha jambo mbele ya Umoja wa Mataifa na majukwaa ya kimataifa, waliksa uungaji mkono hata kutoka kwa waitifaki wake wa kawaida wa Ulaya.
Dakta Rouhani amesema serikali itafanya kila iwezalo kupunguza makali ya vikwazo vya kiuchumi kwa upande mmoja, na kuhakikisha kuwa vikwazo hivyo vya kidhalimu vinafikia tamati kwa upande mwingine.