Vifo vya corona vyapungua kwa asilimia 70 nchini Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i65631-vifo_vya_corona_vyapungua_kwa_asilimia_70_nchini_iran
Waziri wa Afya wa Iran ametangaza kuwa vifo vinavyosababishwa na virusi vya corona vimepungua kwa asilimia 70 hapa nchini katika kipindi cha siku 45 zilizopita.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jan 07, 2021 04:12 UTC
  • Saeed Namaki
    Saeed Namaki

Waziri wa Afya wa Iran ametangaza kuwa vifo vinavyosababishwa na virusi vya corona vimepungua kwa asilimia 70 hapa nchini katika kipindi cha siku 45 zilizopita.

Saeed Namaki amesema kuwa mwenendo wa kupungua vifo vya waathirika wa corona unaendelea hapa nchini na kuongeza kuwa, kutokana na ushirikiano mkubwa wa wananchi na taasisi nyingine, kiwango cha kulazwa watu mahospitalini kutokana na maambukizi ya corona hapa nchini pia kimefikia robo katika siku 45 zilizopita.

Waziri wa Afya wa Iran amesema kuwa, kwa mujibu wa tathmini za kimataifa, vifo vya wagonjwa wa corona katika wimbi la tatu la maambukizi ya virusi hivyo katika nchi zilizoendelea za Ulaya vitafikia watu elfu moja kwa siku na huko Marekani vinakadiriwa kuwa vifo vya watu elfu 2500 na Iran watu 1200 kwa siku; lakini habari njema ni kwamba, utabiri huo haukutimia hapa nchini Iran. 

Madaktari na wauguzi wa Iran wakipambana na corona

Namaki amesema mtu wa pili anayeshukiwa kuwa na aina mpya ya kirusi cha corona iliyoanzia Uingereza amefanyiwa vipimo na kuongeza kuwa: Kwa bahati nzuri hadi sasa mtu mmoja tu ndiye aliyegunduliwa kuwa na kirusi cha aina hiyo hapa nchini na hali yake inaendelea vizuri. 

Watu 82 wameaga dunia nchini Iran katika masaa 24 yaliyopita kutokana na ugonjwa wa Covid-19 na wengine karibu elfu sita wameambukizwa virusi hivyo.