Iran yaiandikia barua WHO kulalamikia vikwazo vya kidhalimu vya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i57587-iran_yaiandikia_barua_who_kulalamikia_vikwazo_vya_kidhalimu_vya_marekani
Waziri wa Afya wa Iran amemuandikia barua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) akimtaka asinyamaze kimya mbele ya vikwazo vya Marekani dhidi ya watu wa Iran katika kununua dawa, chakula na bidhaa za kitiba.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 30, 2019 04:05 UTC
  • Iran yaiandikia barua WHO kulalamikia vikwazo vya kidhalimu vya Marekani

Waziri wa Afya wa Iran amemuandikia barua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) akimtaka asinyamaze kimya mbele ya vikwazo vya Marekani dhidi ya watu wa Iran katika kununua dawa, chakula na bidhaa za kitiba.

Katika barua yake kwa Daktari Tedros Adhanom Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Waziri wa Afya wa Iran Daktari Saeed Namaki amesema: "Marekani inadai kuwa vikwazo vyake dhidi ya Iran havijumuishi dawa, chakula na bidhaa za tiba lakini kivitendo, imechukua hatua za makusudi za kuzuia dawa kuwafikia watu wa Iran kutoka nje ya nchi."

Daktari Namaki amesema vikwazo vya Marekani dhidi ya watu wa Iran si tu kuwa ni ugaidi wa kiuchumi bali pia ni jinai dhidi ya binadamu. Ameongeza kuwa, kuweka vizingiti katika ununuzi wa dawa na vifaa vya kitiba ni jambo ambalo limeathiri vibaya kiwango cha matibabu kwa wagonjwa wengi nchini Iran. Waziri wa Afya wa Iran amesema hatua ambazo Marekani imechukua katika kuwawekea vikwazo watu wa Iran ni kinyume cha malengo ya dunia ya kuwapa watu wote huduma za afya.

Daktari Tedros Adhanom Mkurugenzi Mkuu wa WHO

Amesema katika vikwazo vyake dhidi ya Iran, Marekani imekiuka sheria na mikataba ya kimataifa.

Daktari Namaki ameendelea kusema kuwa, WHO kama mhusika mkuu katika utekelezaji wa mpango wa afya kwa wote duniani haipaswi kukaa kimya mbele ya jinai za Marekani. Ameongeza kuwa wakuu wa Umoja wa Mataifa wanapaswa kukabiliana na vitendo vya ukiukwaji wa sheria vinavotekelezwa na Marekani hasa ukiukwaji wa haki za binadamu.