Mtoto mmoja hufariki dunia nchini Yemen kila baada ya dakika tano
Msemaji wa Wizara ya Afya ya Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen, amesema kuwa, mtoto mmoja hufariki dunia nchini Yemen kila baada ya dakikat tano kutokana na utapiamlo na magonjwa mengine ya kuambukiza.
Yusuf Al-Hadhiri, Msemaji wa Wizara ya Afya ya Yemen aliyasema hayo Jumanne akielezea hali mbaya ya kibinaadamu nchini humo na kuitaja kuwa ya mgogoro, na kuutaka muungano vamizi wa Saudi Arabia uhitimishe mzingiro wake dhidi ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa duru za kidaktari nchini Yemen, katika mwezi uliopita wa Mei karibu Wayemen 2000 walifariki dunia katika mji wa Aden, kusini mwa nchi hiyo kutokana na magonjwa ya kuambukiza ukiwemo ugonjwa wa Covid-19.
Ripoti hiyo imeongeza kwamba tarehe mosi Juni watu 61 walifariki dunia kutokana na maambukizi ya virusi vya homa kali, Corona na Malaria katika mji wa Aden. Hii ni katika hali ambayo kabla ya hapo Shirika la Afya Duniani (WHO) pia lilionya juu ya matokeo mabaya ya kuenea kwa virusi vya Corona nchini Yemen. Saudia, Imarati na nchi nyingine zilianzisha mashambulizi makali na mzingiro wa kila upande dhidi ya Yemen kuanzia mwezi Machi mwaka 2015. Hadi sasa zaidi ya Wayemen elfu 16 wameuawa, makumi ya maelfu kujeruhiwa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.