Rabiei: Utekelezaji wa JCPOA hauhitaji mazungumzo mengine
-
Ali Rabiei
Msemaji wa serikali ya Iran amezungumzia udharura wa Marekani kusitisha ukiukaji wa majukumu yake ya kimataifa na kueleza kuwa hakuna haja ya kufanya mazungumzo mengine kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake ndani ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Akizungumza na waandishi habari kuhusu uwezekano wa Iran kufanya mazungumzo na Marekani baada ya kuingia madarakani Joe Biden, Ali Rabiei amesema kuwa: Utekelezaji wa majukumu ya nchi haupasi kuwa mada ya mazungumzo, na Iran pia imeeleza mara kadhaa kwamba iwapo Marekani itatekeleza majukumu yake na kuondoa vikwazo, Tehran pia itarejea katika utekelezaji kamili wa majukumu yake ndani ya makubaliano ya JCPOA.
Rabiei ameongeza kuwa, baadhi ya nchi za Magharibi zinataka kujadili upya baadhi ya masuala yaliyojadiliwa na kupasishwa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA jambo ambalo haliwezekani; na Iran, China na Russia zimepinga waziwazi jambo hilo.
Msemaji wa serikali ya Iran ameeleza kuwa, tangu hapo awali Tehran iliikosoa serikali ya Donald Trump kuhusu taathira za hatua zake na kujichukulia maamuzi ya upande moja na kuongeza kuwa: Gharama za kukaa kimya wakosoaji wa Trump na kukubaliana na sera zake dhidi ya Iran ndani ya Marekani hatimaye zimewarudia Wamarekani wenyewe nchini kwao.