Zarif: Matukio ya kimataifa hayaathiri uhusiano wa kistratijia wa Iran-China
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i66936-zarif_matukio_ya_kimataifa_hayaathiri_uhusiano_wa_kistratijia_wa_iran_china
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amepongeza 'ushirika wa kistratijia' wa Iran na China na kuongeza kuwa, matukio ya kimataifa hayawezi kuathiri urafiki baina ya washirika hawa wawili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 16, 2021 22:57 UTC
  • Zarif: Matukio ya kimataifa hayaathiri uhusiano wa kistratijia wa Iran-China

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amepongeza 'ushirika wa kistratijia' wa Iran na China na kuongeza kuwa, matukio ya kimataifa hayawezi kuathiri urafiki baina ya washirika hawa wawili.

Zarif ameyasema hayo katika makala aliyoiandika katika gazeti la China la The People's Daily Jumanne kwa mnasaba wa mwaka wa 50 wa kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya Iran na China.

Aidha amesema mabadilishano baina ya China na Iran yana historia ndefu na kuongeza kuwa, nchi hizi mbili zinadumisha uhusiano wa kibiashara na kiutamaduni kupitia Njia ya Hariri, ambayo ni njia ya kale ya kibiashara.

Mpango wa China wa Ukanda na Barabara (BRI)

Halikadhalika Zarif amesema nchi mbili zinafungamana na sera huru za kigeni na zinafuatilia ushirikiano wa kiuchumi sambamba na kuungana mkono katika masuala mbali mbali ya kimataifa.

Zarifu ameelezea matumaini kuwa Iran itakuwa na anfasi kubwa zaidi katika Mpango wa China wa Ukanda na Barabara (BRI) ambao ni mpango wa ustawi wa miundo msingi ya kistratijia wa kuuganisha mabara ya Asia, Ulaya na Afrika.

Hivi karibuni Iran na China zimekuwa zikifanya mazungumzo kwa lengo la kusaini mapatano ya ushirikiano wa muda mrefu.