Zarif alaani nchi za Magharibi zilizompa Saddam silaha za sumu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amezilaani nchi za Magharibi ambazo zilimpa dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein silaha za sumu. Amesema nchi hizo hazijali kukumbuka mauaji ya umati ya watu wa Iraq ambao waliuawa kwa silaha hizo za maangamizi ya umati.
Katika ujumbe kupitia ukurasa wake wa Twitter Jumatatu, Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameandika: "Machi 16 ni kumbukumbu ya mwaka wa 33 wa mauji ya watu wa Halabja kwa silaha za sumu."
Ameongeza kuwa, "Baadhi katika nchi za Magharibi, ambao walimpa Saddam silaha angamizi za sumu, hawajajali kukumbuka tukio hilo."
Aidha Zarif ameongeza kuwa: "Zaidi ya raia 5,000 wasio na hatia waliuawa kwa gesi ya sumu." Amesema ni aibu kuwa nchi za Magharibi ambazo zilimpa Saddam silaha hizo za sumu sasa zinathubutu kudai kuwa eti Iran inavuruga uthabiti katika eneo, ili kufunika jinai zao.
Ikumbukwe kuwa, miaka 33 iliyopita mwezi huu wa Machi, utawala wa zamani wa Baath huko Iraq uliushambulia mji wa Wakurdi wa Halabja huko kaskazini mashariki mwa Iraq. Makumi ya ndege za kivita za utawala wa Saddam Hussein zilifanya mashambulizi ya kinyama kwa kutumia silaha za kemikali dhidi ya raia wa Kikurdi wa mji wa Halabja.
Utawala wa Baath ulianzisha mashambulizi hayo katika hali ambayo kwa upande mmoja utawala huo ulikuwa umeshindwa kukabiliana na wapiganaji wa Kiislamu wa Iran na wa Kikurdi wa Iraq na kwa upande wa pili wananchi Waislamu wa Halabja waliwakaribisha na kuwaunga mkono wapiganaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na dhulma na ukandamizaji usio na kipimo waliokuwa wakifanyiwa na Saddam Hussein.
Nchi za Magharibi ambazo ndizo zilizoupatia utawala wa Saddam teknolojia na nyenzo zinazohitajika kwa ajili ya uzalishaji wa silaha hizo za kemikali, hazikuchukua hatua yoyote ya kivitendo mbele ya jinai hizo za Saddam Hussein, licha ya karibu watu elfu tano kuuawa katika maafa hayo ya kutisha ya Halabcha.