Iran: Nchi zinazokanyaga haki za mataifa mengine hazipaswi kujifanya zinaheshimu haki hizo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i68246-iran_nchi_zinazokanyaga_haki_za_mataifa_mengine_hazipaswi_kujifanya_zinaheshimu_haki_hizo
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amejibu azimio dhidi ya Iran lililotolewa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa, nchi zinazokanyaga haki za mataifa ya dunia hazina ustahiki wa kuzungumzia haki za binadamu.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Mar 24, 2021 02:34 UTC
  • Iran: Nchi zinazokanyaga haki za mataifa mengine hazipaswi kujifanya zinaheshimu haki hizo

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amejibu azimio dhidi ya Iran lililotolewa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa, nchi zinazokanyaga haki za mataifa ya dunia hazina ustahiki wa kuzungumzia haki za binadamu.

Saeid Khatibzadeh amesema hayo leo (Jumatano) wakati akijibu azimio lililotolewa na kundi moja la nchi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kikao cha 46 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, azimio hilo limekosa kura zinazotakiwa, ni dhaifu na halikukubaliwa kimataifa.

Amesema, azimio hilo ni la muendelezo wa ripoti tu za ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa ambaye katika ripoti zake za huko nyuma alishindwa hata kugusia mauaji ya makumi ya watoto wasio na ulinzi na sauti za kuomba misaada za mamia ya wagonjwa wasio na hatia ambao wanashindwa kupata madawa na vifaa vya matibabu. Ripoti zake zimeshindwa angalau kugusia uvunjaji mkubwa wa haki ya kuishi na haki ya kupata matibabu maelfu ya wananchi wa Iran kutokana na vikwazo vya kidhulma vilivyowekwa na maadui.

Jinai wanazofanyiwa wananchi wa Yemen kwa kutumia silaha za Marekani na watenda jinai wenzake ni kubwa, lakini ripota wa Umoja wa Mataifa ameshindwa hata kuligusia hilo katika ripoti zake

 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia amesema, waliounga mkono azimio hilo, yaani Marekani na watenda jinai wenzake, ndio wanaolifanyia taifa la Iran ugaidi mkubwa wa kiuchumi na vikwazo vya kiwango cha juu na vya kidhalimu ambavyo vimepiga marufuku hata kufika madawa nchini Iran tena wakati wa janga la dunia nzima la ugonjwa hatari wa COVID-19.

Amesema, pamoja na dhulma yote hiyo inayofanyiwa, lakini muda wote Iran imetekeleza vizuri majukumu yake ya kulinda haki za wananchi wake na za jamii ya kimataifa.