Jenerali Salami: Kikosi cha Quds kimevuruga dira ya maadui
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (IRGC) amesema Kikosi cha Quds cha Jeshi la SEPAH kimevuruga na kusambaratisha dira, maono na nguvu za madola ya kiistikbari kwa kuimarisha uwezo wake wa kujihami na kushambulia.
Brigedia Jenerali Hossein Salami alisema hayo jana Jumatano katika hafla ya kumuarifisha Naibu Kamanda mpya wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la IRGC, Brigedia Jenerali Mohammad Reza Fallahzadeh, ambaye amechukua nafasi ya Shahidi Mohammad Hosseinzadeh Hijazi, ambaye aliaga dunia hivi karibuni akiwa na umri wa miaka 65, kutokana na mshtuko wa moyo.
Jenerali Salami amebainisha kuwa, Kikosi cha Quds cha SEPAH ya Iran kinafuatilia stratejia ya kujiimarisha barabara na kukifanya kiwe kikosi cha kutegemewa. Amesema uwezo mkubwa usio na kifani wa Kikosi cha Quds umesambaratisha njama za madola ya kibeberu za kuugawanya umma wa Kiislamu.
Aidha Kamanda Salami ameeleza bayana kuwa, Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la SEPAH anaenziwa na kuheshimiwa sana na taifa la Iran.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa Shahidi Soleimani ana nafasi ya kipekee katika nyoyo za wananchi wa Iran na ni muhali kumtenganisha na nafsi za Wairani.
Kadhalika Brigedia Jenerali Hossein Salami amesisitiza kuwa, Kikosi cha Quds kimevuruga kikamilifu dira na maono ya maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kutokana na uwezo wake mkubwa wa kujihami.