Jun 03, 2021 04:15 UTC
  • Wagombea urais nchini Iran kushiriki katika midahalo mitatu

Tume ya Kampeni za Uchaguzi za Wagombea Urais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa midahalo mitatu itayowashirikisha wagombea wote saba itafanyika katika kipindi cha siku chache zijazo.

Tume hiyo ambayo mwenyekiti wake pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani Bw. Abdul-Ridha Rahmani Fazli, imetangaza tarehe mpya za mdahalo huo ambao utarushwa mubashara na televisheni ya taifa ya Iran. Taarifa zinasema, mdahalo wa kwanza utafanyika Jumamosi Juni 5,  wa pili Jumanne Juni 8 na mdahalo wa tatu Jumamosi 12 Juni.

Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) linatayarisha mdahalo huo ambao utawashirikisha wagombea wote saba wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Kiislamu.

Wagombea urais katika uchaguzi wa mwaka huu nchini Iran ni Saeed Jalili, Mohsen Rezaee Mirgha'ed, Sayyid Ebrahim Raisi, Alireza Zakani, Sayyid Amir-Hossein Ghazizadeh Hashemi, Mohsen Mehralizadeh na Abdolnaser Hemmati.

Rais wa sasa Hassan Rouhani anakamilisha muhula wake wa pili mfululizo na hivyo haruhusiwi kugombea awamu hii kisheria.

Kwa mujibu wa sheria za uchaguzi nchini Iran, kampeni za uchaguzi za wagombea wa urais zilianza rasmi tarehe 25 Mei ambapo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran ilitangazwa majina ya wagombea. Kampeni hizo zinaendelea hadi masaa 24 kabla ya kuanza zoezi la kupiga kura.

Wagombea wote nchini Iran wanapewa haki sawa kwa kuhesabiwa mpaka sekunde za kufanya kampeni katika Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, bila ya kupunguziwa au kuongezewa hata sekunde moja. 

Uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na uchaguzi wa 6 wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji unatarajiwa kufanyika Ijumaa ya tarehe  18 mwezi ujao wa Juni, 2021.

Tags