Taifa la Iran katika mtihani mwingine wa uchaguzi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i71326-taifa_la_iran_katika_mtihani_mwingine_wa_uchaguzi
Taifa la Iran siku mbili zijazo litashiriki katika uchaguzi muhimu wa rais na mabaraza ya miji na vijiji. Zoezi la uchaguzi siku zote hufuatiwa na mabadiliko ambayo yumkini yakawa chachu ya harakati kubwa ya jamii kuelekea kwenye ustawi na maendeleo zaidi.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Jun 16, 2021 04:33 UTC
  • Taifa la Iran katika mtihani mwingine wa uchaguzi

Taifa la Iran siku mbili zijazo litashiriki katika uchaguzi muhimu wa rais na mabaraza ya miji na vijiji. Zoezi la uchaguzi siku zote hufuatiwa na mabadiliko ambayo yumkini yakawa chachu ya harakati kubwa ya jamii kuelekea kwenye ustawi na maendeleo zaidi.

Wagombea 7 wanaochuana katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais nchini Iran wameonyesha katika kampeni na midahalo ya uchaguzi kwamba, wote wanakutana katika nukta moja muhimu, nayo ni kufanya mageuzi katika mitazamo kwa kutumia fursa zilizopo, iwapo watahabatika kushinda nafasi hiyo. Kila mmoja kati ya wagombea hao ametangaza sera na mipango yake kuhusu jinsi ya kupunguza matatizo yaliyopo, koboresha uchumi na kulinda hadhi na heshima ya taifa kikanda na kimataifa. Wagombea karibu wote wanasisitiza kwamba, mipango na sera zao zinatekelezeka sambamba na kutilia mkazo udharura wa kilindwa hadhi na usalama wa kitaifa katika mambo yote. Vilevile wameahidi kuunda serikali imara na madubuti, inayochapakazi na yenye ufanisi. Midahalo na kampeni za uchaguzi wa rais hapa nchini pia imejadili vipaumbele vya siasa za nje za Iran na jinsi ya kuwa na mahusiano na nchi nyingine sambamba na kulinda heshima na misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Wagombea katika uchaguzi wa rais nchini Iran

Inatupasa kusema hapa kuwa, uchaguzi ni mchakato wenye pande mbili; upande wa wagombea na ule wa wapigakura ambao kimsingi ndio nguzo kuu katika utawala wowote wa kidemokrasia. Kwa msingi huo, kila mgombea anawajibika kufanya jitihada kubwa za kuwashawishi wapigakura kwa ajili ya kupata tiketi ya kuongoza nchi hii kwa kipindi cha miaka minne ijayo. Hata hivyo kupata ushindi katika kinyang'anyiro hicho si jambo rahisi na jepesi.

Hasa ikitiliwa maanani kwamba, wagombea wamezungumzia na kutoa maoni mengi kuhusu masuala ya uchumi, maisha ya wananchi, ajira, maskani, kupambana na ufisadi na ubaguzi na kadhalika lakini jambo muhimu zaidi ni kuchagua mtu anayefaa kwa ajili ya kutekeleza yanayosemwa na kupigiwa debe. Hali hiyo ilishuhudiwa pia katika uchaguzi uliopita wa rais ambapo baadhi ya mambo yaliyosemwa na kuahidiwa katika kampeni za uchaguzi hayakutekelezwa kutokana na kutokuwa na tabiri au udhaifu wa uongozi wa baadhi ya maafisa wa serikali. Matokeo yake ni mfumuko wa bei, uhaba wa baadhi ya bidhaa muhimu na matatizo ya kiuchumi na uzalishaji wa taifa ambavyo athari zake zinashuhudiwa hivi sasa katika baadhi ya sekta hapa nchini.

Kwa kutilia maanani hayo yote uchaguzi wa rais wa Ijumaa ijayo unaweza kuwa mwanzo wa mageuzi katika utendaji wa serikali. Vilevile yumkini hali hiyo tuliyoizungumzia punde ikawa sababu ya kupungua ushiriki wa wananchi katika zoezi la kupiga kura. Yote hayo mawili yana faida na hasara zake. Kushiriki kwa wingi wananchi katika kupiga kura kuna umuhimu kwa sababu kuchagua ni haki ya kila mwananchi, na kila kura inayopigwa ina taathira chanya katika kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa. Kupuuzwa kwa haki hiyo ya kupiga kura pia kutakuwa na maana ya kutojali na kutokuupa umuhimu mustakbali wa taifa, suala ambalo bila shaka litakuwa na taathira mbaya na za muda mrefu.

Ukurasa rasmi wa Ayatullah Ali Khamenei katika mtandao ya kijamii wa Twitter umeandika kuwa: “Wakati mwingine kura moja tu huwa na taathira kubwa na muhimu sana; hivyo si sahihi kwa mtu kusema: Kura yangu moja haitabadili chochote. Yumkini kura moja au kura kadhaa zikabadili kabisa mustakbali wa taifa.”

Tajiriba ya huko nyuma imeonesha kuwa, iwapo mshindi wa uchaguzi wa rais hatalipa kipaumbele suala la uchapakazi na utendaji tangu baada tu ya kushika madaraka, basi hataweza kutimiza malengo na ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi.