Ijumaa 18 Juni, Siku ya Uchaguzi Nchini Iran
Leo kote Iran kumefanyika uchaguzi wa 13 wa rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, pamoja na uchaguzi mdogo wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), uchaguzi mdogo la Baraza la Wataalamu na uchaguzi wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo saa moja asubuhi alifika katika kituo cha kupigia kura katika ukumbi wa Husainiya ya Imam Khomeini (MA) mjini Tehran na baada ya kupiga kura alizungumza na taifa la Iran na kusema: "Leo wananchi ndio wenye uwanja na medani na kwa kura zao wanaainisha ramani ya nchi kwa ajili ya miaka kadhaa ijayo, hivyo leo ni siku yao."
Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa: "Akili na mantiki vinahukumu kwamba wananchi wote wanapaswa kushiriki katika mtihani huu mkubwa wa kitaifa na kwamba zoezi hili la kuchagua rais linawafaidisha wananchi wenyewe na kuipaisha juu Jamhuri ya Kiislamu katika medani za kimataifa. Kura ya kila raia ina umuhimu mkubwa." Aidha amesisitiza kuwa, wote wanapaswa kupiga kura na mtu hapaswi kusema kura yake moja haitakuwa na faida kwani ni hiyo kura moja ambayo ikijumuishwa na kura zingine huwa ni mamilioni ya kura za wananchi.
Uchaguzi wa leo Ijumaa sawa na chaguzi zingine zoote katika kipindi cha miaka 42 iliyopita tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, una umuhimu mkubwa. Hapa tunaweza kuashiria nukta tatu ambazo zinazingatiwa zaidi.
Kwanza ni kuhusu umuhimu wa uchaguzi na kuendelezwa mfumo wa demokrasia ambapo kura ya wananchi inatumika kuainisha hatima ya nchi. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, uchaguzi daima umekuwa nguzo muhimu ya kuimarisha demokrasia na pia uchaguzi umekuwa ukitoa fursa ya kuwepo makundi yenye mitazamo mbali mbali ya kisiasa. Mitazamo inayotafautiana kisiasa ni ishara ya kuwepo uchaguzi salama na ni nukta muhimu katika kila uchaguzi.
Nukta ya pili ni kuwa, umuhimu wa uchaguzi na taathira zake za kisiasa na kijamii hutokana na kushiriki wananchi.
Kwa msingi huo, kushiriki katika uchaguzi ni kutekeleza wajibu wa kidini na ni haki ya kisiasa na kijamii. Haki hii ina taathira pana sana ambazo ni zaidi ya haki ya mtu binaafsi tu kwani kila kura inayopigwa hatima hujumuisha mamilioni ya kura za wananchi ambazo huleta mshikamano wa kisiasa na umoja wa kitaifa na kidini. Kwa msingi huo ushiriki mdogo katika uchaguzi ni jambo linaloweza kuwa na taathira hasi katika mustakabali wa kisiasa wa nchi.
Kwa maelezo hayo, nukta ya tatu kuhusu umuhimu wa uchaguzi ni taathira yake katika kuimarisha nguzo za mfumo wa Kiislamu.
Uzoefu unaonyesha kuwa, katika chaguzi 38 ambazo zimefanyika Iran tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kila mara wakati kunakua na ushiriki mkubwa wa wananchi katika uchaguzi, taathira zake huwa ni kubwa katika nyuga za kisiasa, kijamii na kiuchumi.
Iran ni nchi kubwa na yenye uwezo wa kiwango cha juu. Kwa hivyo kumchagua rais mwenye uwezo na mtendaji kazi kunaweza kutoa mchango mkubwa katika kustawisha nchi hadi kiwango cha juu kabisa. Uchaguzi wa busara utapelekea kufikiwa malengo muhimu ya kitaifa ili nchi iweze kufikia malengo yake ya ustawi.
Kile kilichowazi ni kuwa, pamoja na kuwepo panda shuka katika mchakato mzima wa uchaguzi, lakini nukta muhimu ni kuwa uchaguzi sahihi huleta mabadiliko bora katika jamii. Taifa adhimu la Iran limeonyesha mara kadhaa kuwa, hutumia busara na hekima katika uchaguzi na hivyo kuchagua watu wanaostahiki ili nchi iweze kuchukua hatua kubwa zaidi katika ustawi na maendeleo. Uchaguzi wa leo Ijumaa una sifa hiyo hiyo.