Rais Nicolas Maduro apongeza ushindi wa Ayatullah Raisi katika uchaguzi wa Rais
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i71468-rais_nicolas_maduro_apongeza_ushindi_wa_ayatullah_raisi_katika_uchaguzi_wa_rais
Rais wa Venezuela ametuma ujumbe akimpongeza Sayyid Ibrahim Raisi kwa kuibuka mshindi katika uchaguzi wa rais hapa nchini na ametoa wito wa kuboreshwa zaidi uhusiano kati ya nchi mbili.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Jun 20, 2021 03:44 UTC
  • Rais Nicolas Maduro apongeza ushindi wa Ayatullah Raisi katika uchaguzi wa Rais

Rais wa Venezuela ametuma ujumbe akimpongeza Sayyid Ibrahim Raisi kwa kuibuka mshindi katika uchaguzi wa rais hapa nchini na ametoa wito wa kuboreshwa zaidi uhusiano kati ya nchi mbili.

Duru ya 13 ya uchaguzi wa Rais wa Iran ilifanyika juzi Ijumaa kote nchini na katika nchi 133 za nje kwa ajili ya kumchagua Rais wa nane wa Iran. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran imetangaza kuwa, Sayyid Ibrahim Raisi ameshinda uchaguzi wa rais wa juzi kwa kupata zaidi ya kura milioni 17 na laki tisa. 

Shirika la habari la FARS pia limeripoti kuwa, Rais Nicolas Maduro pia ametuma ujumbe kwa wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiwapongeza kwa kushiriki kwa wingi katika uchaguzi wa Rais wa juzi Ijumaa. 

Rais Maduro ametoa mkono wa pongezi kwa  Sayyid Ibrahim  Raisi kwa kuibuka na ushindi katika duru ya 13 ya uchaguzi wa Rais na kueleza kuwa, rais mteule Ibrahim Raisi na wananchi wanamapinduzi wa Iran wanaungwa mkono kikamilifu na Mapinduzi ya Kibolivari ili kupanua umoja wa watu wa nchi mbili kwa ajili ya mapambano ya kutetea haki za raia, heshima na mamlaka ya kujitawala katika siku za usoni kwenye ulimwengu huu wenye migogoro. 

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela 

Kabla ya pongezi hizi za Rais wa Venezuela pia, Sayyid Hassan Nasrullah Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Rais Vladimir Putin wa Russia, Rais Recep Tayyeb Erdogan wa Uturuki, Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan, Rais wa Iraq Barhum Saleh na Mustafa Kadhimi Waziri Mkuu wa nchi hiyo  na wengineo walikuwa tayari wametuma jumbe kwa nyakati tofauti wakipongeza ushindi wa Ayatullah Raisi katika uchaguzi wa Rais wa Iran.