Araqchi: Inachotaka Iran ni kuondolewa vikwazo vyote vya Marekani
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kwa kusisitiza kwamba inachotaka Tehran ni kufutwa vikwazo vyote vya Marekani na msimamo huo kamwe hautobadilika.
Sayyid Abbas Araqchi alisema hayo jana baada ya kikao cha kamati ya pamoja ya na makubaliano ya JCPOA kilichofanyika Vienna Austria na kusema kuwa, tumekaribia kufika mwisho wa safari, hata hivyo masafa yaliyobakia hayatokuwa rahisi.
Ameongeza kuwa, katika kikao cha kamati hiyo ya pamoja, pande husika zimefanya mazungumzo ya kina na magumu kuhusu muhtasari wa maafikiano yaliyofikiwa hadi hivi sasa.
Araqchi ambaye pia ni mkuu wa timu ya Iran ya mazungumzo katika kamati hiyo ya pamoja na JCPOA vile vile amesema kuwa, wajumbe wa pande zote wamekiri kwamba kumepatikana maendeleo mazuri kwenye mazungumzo hayo na kila mmoja ameonesha nia ya kweli ya kutaka kufikiwa makublaiano kamili. Pamoja na hayo amesema, bado kuna masuala ya kimsingi ambayo inabidi wachukuaji maamuzi katika nchi husika wayajadili ya kutangaza misimamo yao.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran vile vile amekumbusha kuwa, tangu awali msimamo wa Tehran ni kuondolewa vikwazo vyote vya Marekani na msimamo huo haujabadilika hata kidogo.
Mzunguzmo hayo ya JCPOA mjini Vienna yanajumuisha Iran katika upande mmoja na upande wa pili unajumuisha nchi za 4+1 ambazo China, Russia, Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani pamoja na Umoja wa Ulaya.
Hizo ndizo pande zilizobakia katika mapatano ya JCPOA baada ya Marekani kujiondoa katika makubaliano hayo ya kimataifa mwaka 2018. Mwezi Mei mwaka 2018, rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump alijitoa katika mapatano ya JCPOA na kuirejeshea Iran vikwazo vyote vilivyokuwa vimeondolewa baada ya kufikiwa makubaliano hayo. Inachosisitiza hivi sasa Iran ni haki yake ndani ya JCPOA, yaani kuondolewa vikwazo vyote vilivyorejeshwa na Trump baada ya kujitoa.