Iran: Kinachosubiriwa kuhusu mapatano ya JCPOA ni maamuzi ya kisiasa tu
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kilichobakia kuhusu mazungumzo ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA ni maamuzi ya kisiasa tu, na kama wanasiasa watachukua maamuzi sahihi, basi mazungumzo hayo yatakamilika.
Saed Khatibzadeh amesema hayo mbele ya waandishi wa habari na huku akijibu swali la mwandishi wa Iran Press kuhusu matumaini ya kukamilika mazungumzo ya JCPOA yanayoendelea huko Vienna amesema, matini ya makubaliano haina utata wowote na kila kitu kiko wazi.
Amefafanua zaidi kwa kusema, kilichobakia hivi sasa ni maamuzi ya kisiasa tu, na kama wanasiasa watachukua maamuzi sahihi, basi bila ya shaka yoyote mazungumzo hayo yatakamilika.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amegusia pia msimamo wa mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani na kusema kuwa, si Jake Sullivan tu, bali kila mtu anajua kwamba Jamhuri ya Kisilamu ya Iran ina msimamo mmoja wa kwamba kamwe haikubali kufanya mazungumzo kuhusu JCPOA mpya isiyokuwa hii iliyopo hivi sasa.
Amesisitiza kuwa, utekelezaji wa mapatano yaliyopo ya JCPOA unaweza kuwapa yakini watu wote kwamba mradi ya nyuklia wa Iran ni wa amani kikamilifu, hivyo lililo muhimu ni utekelezaji wa mapatano yaliyopo ya JCPOA si kutafuta visingizio vya kukwepa utekelezaji wake.
Vile vile Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amejibu swali la mwandishi wa Iran Press kuhusu ajali ya ndege ya Ukraine hapa Tehran na kusema kuwa, ripoti ya kiufundi ya Iran iko kamili na inatoa maelezo ya kina kuhusu ajali hiyo.