Iran inaendelea kuuza nje mafuta yake licha ya vikwazo vya Marekani
Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, licha ya kuweko vikwazo vikali vya Marekani dhidi ya Iran, lakini Tehran inaendelea kuzalisha na kuuza nje mafuta yake.
Bijan Namdar Zangeneh amesema hayo katika kikao cha 181 cha OPEC na kuongeza kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Iran iko chini ya vikwazo na mashinikizo makubwa mno ya Marekani na licha ya kwamba vikwazo hivyo vimeisababishia matatizo sekta ya mafuta, lakini uzalishaji na usafirishaji nje mafuta unaendelea.
Waziri wa Mafuta wa Iran pia amesema kuwa, OPEC ndiyo taasisi pekee ya kiuchumi kwa nchi zinazoendelea na ina taathira za moja kwa moja kwa uchumi wa dunia.
Vile vile amesema, siasa za Iran zimejikita kwenye kuimarisha ushirikiano na misimamo ya pamoja ya nchi wanachama wa OPEC na kuweko ushirikiano baina ya wazalishaji na watumiaji wa nishati ya mafuta.
Bw. Zangeneh pia amesema, Iran imekuwa chini ya mashinikizo makubwa mno ya Marekani katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, sekta yake ya mafuta imepata madhara, lakini Wairani bado wako hai na kamwe hawawezi kusalimu amri mbele ya mashinikizo ya maadui.
Amma katika kuthibitisha kuwa uchumi wa Iran hautegemea tu mafuta, Rais Hassan Rouhani amesema kuwa, kila mwaka Iran huchimba tani 590 za madini humu nchini na kwamba sekta hiyo ina nafasi muhimu katika kutoa fursa za ajira kwa vijana.
Rais Hassan Rouhani alisema hayo jana hapa mjini Tehran wakati akifungua miradi kadhaa ya Wizara ya Madini na Biashara kwa njia ya video.