Zarif na De Mistura wajadili hali na matukio yanayoendelea kujiri nchini Syria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Muhammad Javad Zarif, na Staffan de Mistura, mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria wamekutana na kufanya mazungumzo kuhusu matukio yanayoendelea kujiri nchini humo.
Zarif, ambaye yuko mjini Vienna, Austria kushiriki kikao cha Kundi la Mawasiliano cha kujadili hali ya Syria amekutana na mwakilishi wa UN nchini Syria ambapo wamejadili na kubadilishana mawazo kuhusu hatua zilizochukuliwa hadi sasa katika upelekaji misaada ya kibinadamu katika maeneo tofauti ya nchi hiyo na vilevile kuhusu taratibu na maandalizi ya kikao hicho cha Kundi la Mawasiliano kuhusu Syria kilichopangwa kufanyika leo.
Kabla ya mazungumzo yake na Staffan de Mistura, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekutana na kufanya mazungumzo pia na Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Julie Bishop.
Mapema katika mazungumzo na waandishi wa habari, Dakta Zarif amesisitiza kwa mara nyengine tena kuwa ni njozi tupu kudhani kwamba mgogoro wa Syria unaweza kutatuliwa kwa mtutu wa bunduki. Amesema, katika kikao cha leo cha Kundi la Mawasiliano kuhusu Syria atatilia mkazo ulazima wa kutekelezwa usitishaji kamili na wa pande zote wa vita lakini bila ya kushirikisha makundi ya kigaidi.../