Salami: Tutatumia uwezo wetu kustawisha Iran
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) Brigedia Jenerali Hussein Salami amesisitiza kuwa, taifa la Iran linamtegemea Mwenyezi Mungu na nguvu zake za ndani na kuongeza kuwa, 'tutatumia uwezo wetu wote kwa ajili ya ustawi wa watu wa Iran."
Akizungumza Jumatatu katika kikao katika 'Kituo cha Imam Hussein AS' ambacho kinalenga kutatua matatizo yaliyojitokeza kutokana na janga la COVID-19. Kamanda Salami ameashiria agizo la hivi karibuni la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu kuchukuliwa hatua za lazima kukabiliana na janga la COVID19 na kusisitiza kuhusu kuwapa misaada ya kimaisha wasojiweza ambao wameathiriwa vibaya na janga hili.
Wiki iliyopita, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alisema, kukabiliana na corona ndilo jambo la kwanza na la haraka zaidi la kushughulikiwa nchini.
Ayatullah Khamenei alitoa agizo hilo alipohutubia taifa kwa njia ya televisheni kuzungumzia hali na mripuko mkubwa wa ugonjwa wa Covid-19 nchini na akasema, kuna ulazima wa kujipanga na kutumia mbinu mpya na madhubuti za kujilinda katika kukabiliana na mabadiliko ya spishi na kasi kubwa ya usambaaji wa kirusi cha corona.
Kamanda Mkuu wa IRGC amesema wananchi wa Iran wana ufahamu mzuri na hivyo wanamuelewa adui na wanadiriki baraka za Uislamu na Kiongozi Muadhamu na wana imani pia kuhusu thawabu zinazotokana na subira.
Hali kadhalika amesema taifa la Iran daima limekuwa likitegemea nguvu zake za ndani na Mwenyezi Mungu. Ameongeza kuwa, kote duniani imebainika wazi kuwa iwapo serikali au nchi itategemea ajinabi basi haitakuwa na msingi imara. Aidha amesema wale wanaotaka kuzungumza na Iran kwa kutumia mbinu zinazotumiwa na watawala wa Marekani basi wafahamu kuwa, taifa la Iran halitatoa muhanga heshima yake kwa lolote lile.