Raisi: Uhusiano wa Iran na Uturuki utaingia katika marhala mpya
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria umuhimu wa uhusiano wa kiuchumi na kibiashara wa Tehran na Ankara na kusema kuwa, kustawi kwa ushirikiano wa pande mbili kutaingia katika hatua mpya karibuni hivi, kwa kufanyika kongamano hapa Tehran.
Sayyid Ebrahim Raisi alisema hayo jana Jumatano jioni katika mazungumzo yake ya simu na Recep Tayyip Erdogan, Rais wa Uturuki na kuongeza kuwa, mkutano wa Iran na Uturuki utakaofanyika hivi karibuni hapa mjini Tehran utafungua ukurasa mpya wa uhusiano wa nchi mbili hizo.
Amegusia kuhusu ushirikiano wa Iran na Uturuki katika vita dhidi ya ugaidi na kusisitiza kuwa, njia kuu ya kukabiliana na harakati za makundi ya kigaidi Asia Magharibi ni kuheshimu mamlaka ya kujitawala nchi za eneo hili.
Sayyid Raisi ameeleza kuwa, Iran imepata mafanikio makubwa katika vita dhidi ya ugaidi na inakaribisha ushirikiano baina yake na nchi zote katika mapambano dhidi ya jinamizi hilo.
Kadhalika Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, matatizo yanayozikabili nchi za eneo yanaweza kupatiwa ufumbuzi na mataifa yenyewe ya ukanda huu pasina uingiliaji wa madola ajinabi.
Kwa upande wake, Recep Tayyip Erdogan, Rais wa Uturuki amesema uhusiano wa Tehran na Ankara hususan katika nyuga za usalama na uchumi una umuhimu mkubwa na kwamba, kuna udharura wa kuendelea kufanyika mikutano ya pande mbili baina ya Iran na Uturuki katika nyuga tofauti.