Rais wa Iran kuitembelea Russia kufuatia mwaliko wa Putin
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anatazamiwa kuitembelea Russia mapema mwaka ujao 2022, kufuatia mwaliko wa mwenzake wa nchi hiyo, Vladimir Putin.
Hayo yalisemwa jana Jumanne na Ali Bahadori Jahromi, msemaji wa serikali ya Iran ambaye alieleza kuwa, Sayyid Ebrahim Raisi anatazamiwa katika safari yake hiyo kufanya mazungumzo na viongozi wa Russia kuhusu njia za kuimarisha uhusiano wa kistratajia wa Moscow na Tehran.
Amesema Rais Putin amemualika Raisi kuitembelea Russia katika fremu ya kuimarisha uhusiano wa kimkakati baina ya nchi mbili hizi, pamoja na uhusiano wa kieneo na kimataifa.
Jahromi amesema Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran, Mohammad Mokhber yupo katika hatua za mwisho za kuandaa safari hiyo ya Rais wa Iran nchini Russia inayotazamiwa kufanyika mwanzoni mwa mwaka ujao 2022.
Jana Jumanne pia, Dmitry Peskov, Msemaji wa Ikulu ya Kremlin ya Russia alisema Moscow na Tehran zinaandaa mazinigira ya kuwa na mawasiliano ya kiwango cha juu zaidi.
Iran na Russia zimefanikiwa kuboresha uhusiano wao wa pande mbili katika nyuga mbalimbali katika miaka ya hivi karibuni, huku Moscow ikiunga mkono sera na misimamo ya Iran kama vile haki ya Tehran ya kustafidi na miradi yake ya nyuklia yenye malengo ya amani.