Dec 31, 2021 12:54 UTC
  • Khatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran atoa onyo kali kwa utawala wa Kizayuni wa Israel

Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran amesema kuwa, kama utawala haramu wa Kizayuni wa Israel utathubutu kufanya kosa dogokabisa, vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vitatoa jibu kali dhidi yake ambalo litakuwa ni la kuumiza.

Ayatullah Ahmad Khatami amesema hayo leo mbele ya hadhara ya waumini waliohudhuria ibada ya kimaanawi na kisiasa ya Swala ya Ijumaa mjini Tehran ambapo sambamba na kuashiria manuva ya kijeshi ya hivi karibuni ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) yaliyopewa jina la Mtume Mtukufu SAW-17 na radiamali ya viongozi wa Israel kwa manuva hayo ya kijeshi amesema kuwa, sera za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni za kujihami na za kumfanya adui asijaribu kulishambulia kijeshi taifa hili.

Hata hivyo, Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran amesema, kama utawala wa Kizayuni wa Israel utafanya kosa dogo kabisa na kufanya hujuma ya kijeshi dhidi ya taifa hili, basi utakabiliwa na jibu kali la makombora ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH).

Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani

 

Ayatullah Ahmad Khatami ameashiria pia kukaribia mwaka wa pili tangu kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) na kusema kuwa, Iran iliizaba kibao Marekani kwa kushambulia kambi yake ya kijeshi ya Ain al-Asad nchini Iraq, lakini kisasi cha mwisho kitakuwa ni kuadhibiwa wale wote waliosababisha mauaji hayo, waliotekeleza na waliotoa ushauri wa kuuawa Luteni Jenerali Qassem Soleimani hususan Trump mtenja jinai ambaye alitangaza wazi kuhusika na jinai hiyo.

Tags