Iran: Uhusiano wetu na Oman ni wa jadi na imara sana
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i79046-iran_uhusiano_wetu_na_oman_ni_wa_jadi_na_imara_sana
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa, uhusiano wa Tehran na Oman ni wa jadi na imara na kwamba siasa za serikali ya Iran zitaendelea kuwa za kupigania uhusiano imara na majirani zake.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 10, 2022 14:03 UTC
  • Iran: Uhusiano wetu na Oman ni wa jadi na imara sana

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa, uhusiano wa Tehran na Oman ni wa jadi na imara na kwamba siasa za serikali ya Iran zitaendelea kuwa za kupigania uhusiano imara na majirani zake.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Hossein Amir-Abdolahian akisema hayo leo Jumatatu mara bada ya kuwasili Muscat, mji mkuu wa Oman na kuongeza kuwa, nia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kutia nguvu kanali ya kuimarisha ushirikiano na uhusiano baian ya nchi zote za Ghuba ya Uajemi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran yuko nchini Oman kwa ziara ya siku moja ya kikazi na kwa ajili ya kuonana na viongozi wa ngazi za juu wa nchi hiyo ndugu. Ajenda kuu ya mazungumzo hayo imetajwa kuwa ni kuimarisha uhusiano wa pande mbili wa kieneo na wa kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hossein Amir-Abdollahian akingia kwenye ndege kwa ajili ya ziara rasmi ya kiserikali

 

Katika ziara yake hiyo huko Oman, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran atafuatilia pia makubaliano ya pande nne yaliyotiwa saini baina ya Iran, Oman, Turkmenistan na Uzbekistan na kujadiliana na viongozi wa Oman juu ya njia za kuyatekeleza kivitendo makubaliano hayo.

Tarehe tatu mwezi huu wa Januari pia, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Oman walifanya mazungumzo ya simu ikiwa ni ishara ya wazi ya kuzidi kuimarika uhusiano wa nchi hizi mbili ndugu za Kiislamu.

Katika mazungumzo hayo ya simu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir Abdolahian na mwenzake wa Oman, Badr bin Hamad al Busaidi walitilia mkazo ushirikiano wa pande mbili katika nyuga zote na katika masuala yanayozihusu nchi hizi mbili ndugu pamoja na masuala ya kieneo na kimataifa.