Rais Raisi aelekea Qatar kuhudhuria kikao cha wakuu wa nchi zinazozalisha gesi
Rais Ebrahim Raisi ameondoka nchini leo kuelekea Doha mji mkuu wa Qatar kwa madhumuni ya kushiriki kikao cha wakuu wa nchi zinazozalisha gesi.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitangaza kila mara na kinagaubaga kuwa iko tayari kuwa na ushirikiano wa karibu zaidi na nchi za eneo na kwamba kustawisha mashusiano na majirani ni miongoni mwa misingi thabiti ya serikali ya 13.
Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuondoka mjini Tehran, Seyyid Ebrahim Raisi amesema kuhusu malengo ya safari yake ya siku mbili nchini Qatar kwamba, safari hiyo imetokana na mwaliko wa Amir wa nchi hiyo na inafanyika kwa malengo mawili.
Raisi ameongeza kuwa, lengo la kwanza ni kustawisha uhusiano wa pande mbili na nchi rafiki, ndugu na jirani ya Qatar; na lengo la pili ni kushiriki katika kikao cha jumuiya ya nchi zinazozalisha na kusafirisha gesi kwa wingi duniani.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, safari hiyo inafanyika kwa msingi wa kuimarisha mawasiliano na nchi za pembeni ya Ghuba ya Uajemi katika mwendelezo wa diplomasia ya ujirani hususan na nchi hizo. Ameongeza kuwa safari hiyo inalenga pia kutumia fursa za Iran na nchi zingine kwa ajili kustawisha uhusiano wa kisiasa na kiuchumi, hususan na Qatar ambayo ina maeneo ya ushirika ya uchimbaji gesi na Jamhuri ya Kiislamu.
Seyyid Ebrahim Raisi ameashiria ushirikiano wa nchi zinazozalisha na kusafirisha gesi na kukumbusha kuwa uundaji wa jumuiya hiyo ulitokana na ubunifu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Jumuiya ya nchi zinazozalisha na kuuza kwa wingi gesi duniani, yaani OPEC-Gas iliasisiwa mwezi Mei mwaka 2001 hapa mjini Tehran; na kwa sasa ina nchi 11 wanachama na nchi sita wanachama watazamaji.../