Khatibzadeh: Iran inasubiri maamuzi ya Ulaya na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i80608-khatibzadeh_iran_inasubiri_maamuzi_ya_ulaya_na_marekani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Iran inasubiri maamuzi ya Ulaya na Marekani kuhusiana na mazungumzo ya kuondolewa Iran vikwazo ambayo yamekuwa yakiendelea huko Vienna, Austria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 21, 2022 07:06 UTC
  • Khatibzadeh: Iran inasubiri maamuzi ya Ulaya na Marekani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Iran inasubiri maamuzi ya Ulaya na Marekani kuhusiana na mazungumzo ya kuondolewa Iran vikwazo ambayo yamekuwa yakiendelea huko Vienna, Austria.

Akizungumza katika mkutano wa kila wiki na waandishi habari mjini Tehran, Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema ujumbe wa Iran katika mazungumzo ya Vienna umewasilisha mapendekezo yake kuhusu masuala yaliyobakia na sasa kile kinachotakiwa kwa upande wa pili ni kuondoa vikwazo kama ilivyoahidiwa kwa maslahi ya kiuchumi ya Iran.

Amesema hatua kubwa zimechukuliwa katika mazungumzo ya Vienna lakini masuala yaliyobakia ni magumu na kinachosubiriwa ni nchi za Ulaya na Marekani kuchukua maamuzi.

Khatibzadeh amebaini kuwa moja ya nukta muhimu ni kuwa upande wa pili utoe dhamana ya kutekeleza ahadi ili Iran ianze kutekeleza tena ahadi zake katika mpango wake wa nyuklia wenye malengo ya amani.

Mazungumzo ya Vienna

Wabunge zaidi ya 250 wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) jana Jumapili waliwaslisha taarifa yao kwa Rais Ebrahim Raisi wakisema kwamba, timu ya mazungumzo ya Iran isisaini mapatano yoyote katika mazungumzo ya Vienna bila ya kupewa dhamana.

Duru ya nane ya mazungumzo ya Vienna kwa ajili ya kuiondolea Iran vikwazo vya kidhalimu na haramu ilianza tena tarehe 8 mwezi huu wa Februari baada ya mapumziko mafupi kwa lengo la kuchukuliwa maamuzi ya kisiasa.  

Awamu hii imeshuhudia maendeleo mazuri kutokana na mapendekezo mazuri ya Iran. Hata hivyo nchi za Magharibi, ikiwemo serikali ya Joe Biden huko Marekani, zinaendelea kutekeleza vikwazo vya utawala wa Donald Trump na ndizo zinazokwamisha makubaliano ya mwisho huko Vienna.