Feb 23, 2022 02:51 UTC
  • Raisi atoa mwito wa kustawishwa uhusiano wa Iran na Msumbiji

Rais Ebrahim Raisi wa Iran ametoa mwito wa kuboreshwa uhusiano wa pande mbili baina ya Jamhuri ya Kiislamu na Msumbiji katika nyuga tofauti.

Rais Raisi alitoa mwito huo jana Jumanne katika mazungumzo yake na mwenzake wa Msumbiji, Filipe Nyusi pambizoni mwa Mkutano wa Jumuiya ya Nchi Zinazouza Nje Gesi Asilia (GECF) uliofanyika katika mji mkuu wa Qatar, Doha.

Sayyid Raisi ameeleza bayana kuwa, Iran ipo tayari kupanua ushirikiano wake wa kiuchumi na kibiashara na nchi za Afrika hususan Msumbiji.

Ameeleza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu vile vile ina azma ya kuzipa nchi za Afrika uzoefu na ujuzi wake wa kiufundi katika nyuga mbalimbali.

Marais na wakuu wa nchi zilizoshiriki Mkutano wa Jumuiya ya Nchi Zinazouza Nje Gesi Asilia (GECF) Doha

Rais wa Iran amesema tangu baada ya Mapinduzi ya Kiislamu, Tehran imekuwa na uhusiano mzuri na mataifa ya Afrika na kuongeza kuwa, atamuagiza Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kuandaa kamisheni ya pamoja ya ushirikiano wa uchumi haraka iwezekanavyo, kwa shabaha ya kupanua zaidi uhusiano wa pande mbili wa Tehran na Maputo.

Kwa upande wake, Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji amesisitizia haja ya kupigwa jeki uhusiano wa nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyuga mbalimbali. 

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alirejea humu nchini jana usiku baada ya ziara hiyo iliyokuwa na mafanikio makubwa katika nchi jirani ya Qatar.

Tags