Ali Shamkhani: Kuna sababu mbalimbali zinazozifanya Iran na Uzbekistan ziwe na ushirikiano
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i81184-ali_shamkhani_kuna_sababu_mbalimbali_zinazozifanya_iran_na_uzbekistan_ziwe_na_ushirikiano
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema kuwa, kuna haja ya kustawishwa uhusiano wa Iran na Uzbekistan katika nyanja mbalimbali.
(last modified 2026-07-02T04:13:23+00:00 )
Mar 09, 2022 04:02 UTC
  • Ali Shamkhani: Kuna sababu mbalimbali zinazozifanya Iran na Uzbekistan ziwe na ushirikiano

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema kuwa, kuna haja ya kustawishwa uhusiano wa Iran na Uzbekistan katika nyanja mbalimbali.

Ali Shamkhani amesema hayo mjini Tashkent katika mazungumzo yake na Luteni Jenerali Makhmudov Victor, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Uzbekistan ambapo wawili hao wamejadili na kubadilishana mawazo kuhusiana na masuala ya pande mbili, kieneo na kimataifa.

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amekumbusha nafasi muhimu ya kijiopolitiki ya Uzbekistan katika Asia ya Kati na kusema kwamba, masuala kama kuzuia kuenea ugaidi na vitendo vya kufurutu ada katika eneo ni miongoni mwa daghadagha na wasiwasi wa pamoja wa nchi mbili hizi.

Admeri Ali Shamkhani amebainisha kuwa, mipaka ya pamoja ya Iran na Uzbekistan na Afghanistan inazalimu kuweko ushirikiano wa pamoja baina ya Tehran na Tashkent kwa ajili ya kukabiliana na matatizo na kurejesha amani na uthabiti nchini Afghanistan.

Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran

 

Kadhalika ameelezea matumaini aliyonayo ya kuongezwa kasi ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara baina ya Iran na Uzbekistan na kusema bayana kwamba, kwa bahati nzuri irada na azma ya marais wa nchi mbili imepelekea kiwango cha ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi hizi mbili kukua kwa 70%.

Kwa upande wake, Luteni Jenerali Makhmudov Victor, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Uzbekistan amesisitiza udharura wa kutekelezwa kivitendo makubaliano yaliyofiikiwa na viongozi wa pande mbili.