Khatibzadeh: Mfumo wa kimataifa unabadilika
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i81304-khatibzadeh_mfumo_wa_kimataifa_unabadilika
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria vita vya Russia na Ukraine na kueleza kuwa mfumo wa kimataifa uko katika hali ya mageuzi na kubadilika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 12, 2022 09:25 UTC
  • Khatibzadeh: Mfumo wa kimataifa unabadilika

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria vita vya Russia na Ukraine na kueleza kuwa mfumo wa kimataifa uko katika hali ya mageuzi na kubadilika.

Miezi iliyopita Russia ilitahadharisha kuhusu kujitanua kwa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) huko Ulaya Mashariki na kutoa mapendekezo kwa Marekani na Nato kwa ajili ya kudhaminiwa usalama wake; hata hivyo mapendekezo hayo yalipingwa.  

Russia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Ukraine Februari 24 mwaka huu kwa amri ya Rais wa nchi hiyo, Vladimir Putin, sambamba na Ukraine kuomba mara kadhaa kujiunga na NATO na kupatiwa misaada ya mamilioni ya dola kutoka nchi za Magharibi. 

Rais Vladimir Putin wa Russia 

Mapigano bado yanaendelea huko Ukraine na leo yameingia katika siku yake ya 17. Shirika la habari la Iran limeripoti kuwa, Saeed Khatibzadeh Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema leo katika Mkutano wa 15 wa Kila Mwaka wa Wanachuo na Wahadhiri wa Kiirani Nje ya Nchi ambao umefanyika huko Mash'had kwamba: Msingi wa vita vya sasa huko Ukraine uliandaliwa miongo mitatu iliyopita lakini moto wake ndio kwanza umewashwa.  

Khatibzadeh amesema sera ya Iran kuhusu vita kati ya Russia na Ukraine ni kutoegemea upande wowote na kwamba Iran inapinga vita vya aina yoyote na vilevile inapinga sera za Marekani na NATO za kutaka kuimeza dunia.