Iran yauonya vikali utawala wa Kizayuni dhidi ya jinai zake za kihaini
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameashiria shambulizi la kigaidi la Israel lililopelekea kuuawa shahidi askari wawili wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) nchini Syria hivi karibuni, na kuuonya vikali utawala huo wa Kizayuni dhidi ya mwenendo wake huo wa kufanya jinai za kihaini.
Majid Takht Ravanchi ametoa indhari hiyo katika barua aliyomtumia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, na Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la umoja huo mnamo Machi 10.
Ameitaka jamii ya kimataifa kuuwajibisha utawala haramu wa Israel kwa hujuma hiyo ya kigaidi iliyopelekea kuuawa shahidi washauri wawili wa kijeshi wa Iran waliokuwa wanaishauri serikali Syria katika kadhia ya vita dhidi ya ugaidi.
Shambulizi la kombora la utawala haramu wa Israel viungani mwa mji mkuu wa Syria, Damascus Jumatatu iliyopita ya Machi 7, liliua shahidi mashujaa wawili wa jeshi hilo, Kanali Ehsan Karbalaeepour na Kanali Morteza Saeednejad, ambao walikuwa walinzi wa Haram Tukufu nchini Syria.
Katika barua hiyo, mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameeleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inalitazama shambulio hilo la kigaidi la Israel kama uchokozi wa kiwango cha juu, uliokusudia kuibua taharuki na kuvuruga jitihada za wanaopambana na ugaidi katika eneo.

Majid Takht Ravanchi amekumbusha kuwa, washauri wa kijeshi wa Iran wapo nchini Syria kwa mwaliko rasmi wa serikali halali ya nchi hiyo ya Rais Bashar al-Assad.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limesisitiza kuwa, hakuna chembe ya shaka kuwa litalipiza kisasi kwa jinai hiyo iliyofanywa na Wazayuni maghasibu.