Raisi: Kimya cha nchi zinazodai kupigania haki za binadamu lazima kilaaniwe
-
Rais Ebrahim Raisi
Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaumu vikali misimamo ya nyuso mbili ya nchi na mashirika yanayodai kupigania haki za binadamu duniani na kusema kuwa, kimya cha nchi na mashirika hayo lazima kilaaniwe.
Jumamosi wiki hii, wizara ya mambo ya ndani ya Saudi Arabia ilitekeleza adhabu ya kifo kwa watu 81 siku moja ikiwa ni uvunjaji wa wazi kabisa wa haki za binadamu.
Ni vyema tukumbushe hapa kwamba, 41 kati ya watu hao 81 waliotekelezewa adhabu ya kifo kwa siku moja huko Saudia, walikuwa ni vijana wa Kishia wa eneo la Qatif la nchi hiyo. Wengi wa vijana hao walikamatwa na serikali ya Saudi Arabia kwa madai tofauti na kusukumwa korokoroni.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Ebrahim Raisi alisema jana (Jumatatu) kuhusu kuuliwa watu hao wasio na hatia kwamba, misimamo ya kundumilakuli ya nchi za Magharibi na kutumia kwa maslahi yao tu suala la haki za binadamu na vile vile kimya cha nchi zinazodai kupigania haki za binadamu mbele ya mauaji kama hayo, ni vitu ambavyo lazima vilaaniwe.
Amesema, misimao hiyo ya nyuso mbili ya nchi za Magharibi imeonesha wazi kuwa lengo la nchi hizo ni kutumia kisiasa tu suala la haki za binadamu ili kutimiza tamaa zao za kiistikbari na kuzishinikiza nchi huru ulimwenguni.
Rais Raisi pia amesema, mashirika ya kimataifa na vyombo huru vya habari pamoja na taasisi zote husika ni wajibu wao kufichua uhalifu huo.