Apr 07, 2022 01:58 UTC
  • Iran yasafirisha nje dozi milioni 4 za chanjo za COVID-19

Mkuu wa Shirika la Dawa na Chakula la Iran (FDA) amesema Jamhuri ya Kiislamu imefanikiwa kuuza nje ya nchi dozi milioni nne za chanjo za kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19 zilizozalishwa hapa nchini.

Bahram Daraei amenukuliwa akisema hayo na shirika la Iran Press na kuongeza kuwa, chanjo za Corona zilizozalishwa hapa nchini tayari zimepata wateja katika msoko ya kimataifa, na tayari taifa hili limesafirisha nje dozi milioni nne za chanjo hizo.

Mkuu wa Shirika la Dawa na Chakula la Iran amesema chanjo ya COVIran Barekat iliyozalishwa humu nchini ipo katika hatua za mwisho za kusajiliwa kimataifa na kuidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Wanasayansi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanazalisha chanjo mbalimbali kwa kutumia teknolojia na utaalamu wa aina tofauti kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19. 

Chanjo za COVIran Barekat, Razi Cov-Pars, Fakhra na Noura, ni miongoni mwa chanjo za ugonjwa wa UVIKO-19 zilizotengenezwa na wataalamu wa Kiirani na ambazo majaribio na usajili wao umefanyika kwa mafanikio.

chanjo ya COVIran Barekat iliyozalishwa humu nchini

Mafanikio makubwa waliyopata wanasayansi na wataalamu wa Iran katika kuzalisha chanjo za corona humu nchini yamepongezwa na duru mbalimbali zenye itibari za kielimu katika kona tofauti za dunia.

Mafanikio hayo yamepatikana huku Iran ikiwa chini ya vikwazo vya kidhalimu na vya kiwango cha juu kabisa ilivyowekewa na Marekani katika nyuga zote, hata za kimatibabu.

Tags