Iran yailaumu Uingereza kwa kuwalazimisha wakimbizi waende nchini Rwanda
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i82568-iran_yailaumu_uingereza_kwa_kuwalazimisha_wakimbizi_waende_nchini_rwanda
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameilaumu serikali ya Uingereza kwa kuwalazimisha wakimbizi walioko nchini humo kwenda nchini Rwanda na amesisitiza kuwa, kufanya hivyo ni kukwepa London majukumu yake ya kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 16, 2022 02:49 UTC
  • Iran yailaumu Uingereza kwa kuwalazimisha wakimbizi waende nchini Rwanda

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameilaumu serikali ya Uingereza kwa kuwalazimisha wakimbizi walioko nchini humo kwenda nchini Rwanda na amesisitiza kuwa, kufanya hivyo ni kukwepa London majukumu yake ya kimataifa.

Saeed Khatibzadeh alisema hayo jana Ijumaa na kuongeza kuwa, kuwalazimisha wakimbizi walioko Uingereza, kuelekea nchini Rwanda kunakanyaga roho na hati ya mkataba wa kulindwa haki za wakimbizi.

Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amesema, mpango wa Uingereza wa kuwahamishia nchi nyingine wakimbizi waliko nchini humo kunakanyaga haki za wakimbizi hao na kunakwenda kinyume na mikataba wa kulindwa haki zao. Vile vile kitendo hicho ni kinyume na maadili na ni kutojali kabisa masuala ya kiutu na kiakhlaki.

Kanali ya English  (Kwa Kifaransa: la Manche)

 

Nao Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa unapinga vikali suala la kupelekwa kwa lazima nchini Rwanda wakimbiziwalioko Uingereza. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limesema katika taarifa yake kwamba linapinga vikali makubaliano ya Uingereza na Rwanda, ambayo yalichapishwa hivi karibuni kwa ajili ya kuwahamishia Rwanda wahamiaji wanaotafuta hifadhi nchini Uingereza.

Ikumbukwe nchi hizo mbili ziko kwenye maeneo tofauti kabisa ya dunia. Masafa yanayozintenganisha Uingereza na Rwanda yanayokadiriwa.kufikia kilomita 4,500.

Makubaliano hayo yenye utata baina ya nchi mbili za Rwanda na Uingereza yamelalamikiwa vikali na wabunge wa nchi hiyo hasa wa chama cha upinzani cha Labour ambao wamesema hayatekelezeki na ni kinyume na maadili. 

Uingereza imefikia makubaliano hayo na serikali ya Kigali baada ya kushindwa kufikia makubaliano kama hayo na nchi za Ghana na Albania. Serikali ya Rwanda itapewa dola milioni 158 na serikali ya Uingereza kwa kukubali kupokea wakimbizi hao.