Kenya na Iran kuimarisha uhusiano wao katika nyuga za utalii na uwekezaji
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Kenya zimeazimia kusaini makubaliano ya maelewano juu ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika nyuga za uwezekaji na utalii.
Hayo yamesemwa na Mehdi Keshavarz, Afisa Mkuu wa Mtendaji wa Shirika la Eneo Huru la Biashara katika Kisiwa cha Kish kilichoko kusini mwa Ghuba ya Uajemi, katika mkutano wake na Joshua Gatimu, Balozi wa Kenya nchini Iran.
Keshavarz amesema Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Kish iko tayari kusaini makubalino na Kituo cha Ubunifu na Teknolojia cha Iran (IHIT) kilichoko katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, kwa shabaha ya kupiga jeki ushirikiano baina ya nchi mbili hizi.
Afisa Mkuu wa Mtendaji wa Shirika la Eneo Huru katika Kisiwa cha Kish amemuasa Balozi wa Kenya mjini Tehran alipe uzito suala la kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa pande mbili katika nyuga za uchumi, biashara na utalii kupitia kisiwa hicho kilichoko katika eneo la Ghuba ya Uajemi.
Aidha amegusia uwezekano wa kuanzishwa safari za moja kwa moja za ndege baina ya Nairobi na Kish kwa lengo la kupanua biashara na utalii baina ya Kenya na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kwa upande wake, Joshua Gatimu, Balozi wa Kenya nchini Iran mbali na kuashiria fursa za utalii katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki, ametoa pendekezo la kuandaliwa mashindano ya pamoja ya mbio za nyika (marathon) kwa ajili ya kuimarisha utalii wa kimichezo.