Kamanda wa IRGC: Siku ya Quds imeunganisha umma wa Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i83054-kamanda_wa_irgc_siku_ya_quds_imeunganisha_umma_wa_kiislamu
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema: "Siku ya Kimataifa ya Quds imeweza kuunganisha umma wa Kiislamu katika kuunga mkono malengo ya taifa la Palestina."
(last modified 2026-07-03T11:45:53+00:00 )
Apr 29, 2022 03:47 UTC
  • Kamanda wa IRGC: Siku ya Quds imeunganisha umma wa Kiislamu

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema: "Siku ya Kimataifa ya Quds imeweza kuunganisha umma wa Kiislamu katika kuunga mkono malengo ya taifa la Palestina."

Meja Jenerali Hossein Salami Kamanda Mkuu wa IRGC ameyasema hayo katika ujumbe alioutuma kwa njia ya video katika kongamano la Kamati ya Siku ya Kimataifa ya Quds katika Ukanda wa Ghaza.

Meja Jenerali Salami ameongeza kuwa, "Siku ya Kimataifa ya Quds ni zawadi kutoka kwa Imam Khomeini, Mwenyezi Mungu Amrehemu, ambayo imepelekea kadhia ya Palestina iwe ni yenye kupewa kipaumbele na kuzingatiwa katika ulimwengu wa Kiislamu."

Kamanda Mkuu wa IRGC amewatumia salamu wanamapambano wote wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi, Ukanda wa Gaza, Quds Tukufu (Jerusalem) na wote walio katika medani ya Jihadi kuulinda Msikiti wa Al Aqsa.

Meja Jenerali Salami ameongeza kuwa: "Ayatulah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliasisi Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa ajili ya kuunga mkono malengo matukufu ya ukombozi wa Palestina. Ameendelea kusema kuwa, kwa himaya ya Kikosi cha Quds cha IRGC, wananchi wa Palestina wameweza kupita vipindi vigumu na kubadilisha mlingano wa nguvu.

Kamanda Mkuu wa IRGC amesisitiza kuwa, mapatano eti ya amani kama yale ya Camp David Accords,  Oslo, Sharm El Sheikh Memorandum n.k hayajaweza na hayataweza kupelekea ardhi za Palestina zikombolewe. Amesema mapatano kama hayo ni njama za Wazayuni za kuhadaa na kudhoofisha harakati za ukombozi wa Palestina.