Jun 23, 2022 03:38 UTC
  • Afisa wa Iran: Ubaguzi umekita mizizi katika historia ya Uingereza

Ubaguzi na udhalilishaji wa binadamu ni mambo yaliyokita mizizi katika historia ya Uingereza. Hayo yamesemwa na Katibu wa Baraza Kuu la Haki za Binadamu la Iran, Kazem Gharibabadi katika ujumbe wake kwa njia ya Twitter.

Kauli ya Gharibabadi imekuja baada ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza kutangaza kuwa, itawapa wakimbizi wote bangili ya kieletroniki ambayo itafuatilia nyendo zao zote. 

Gharibabadi ameashiria sera hiyo mpya ya kibaguzi nchini Uingereza na kusema: "Ubaguzi unaotekelezwa na serikali na kudhalilisha wanaadamu ni mambo ambayo yamekita mizizi katika historia ya Uingereza. Katika nchi hii tunaona upuuzaji kamili na ukiukwaji wa kinyama wa haki za binadamu."

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza imekosolewa vikali kwa kusema kuwa, wakimbizi wanaopangwa kupelekwa Rwanda kwa nguvu na ambao safari yao imeahirishwa kutokana na kesi mahakamani, watakuwa wa kwanza kuvishwa bangili hizo za kieletroniki.

Katibu wa Baraza Kuu la Haki za Binadamu la Iran Kazem Gharibabadi

Kwa mujibu wa mpango wa majaribio ya miezi 12 ambao ulianza wiki iliypopita, wakimbizi wote ambao wanaingia Uingereza kwa njia ya bahari wakitokea Ufaransa, au wanaoingia wakiwa wamepakiwa ndani ya malori sasa watavishwa bangili hizo maalumu ambazo zina mfumo wa GPS unaoiwezesha serikali kuwafuatilia popote walipo.

Hayo yanajiri wakati ambao mpango wa Uingereza wa kuwapelekea wakimbizi Rwanda kwa nguvu bila hiari yao unaendelea kukosolewa vikali. Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Filippo Grandi, ametupilia mbali uamuzi wa serikali ya Uingereza wa kuwahamishia Rwanda watafuta hifadhi wanaokwenda nchini humo huku akisema makubaliano hayo ya kando kati ya nchi mbili hizo ni makosa, na ni sawa na kufungua ukurasa wa giza katika haki za kimataifa za wakimbizi.

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi ameendelea kueleza kuwa, Rwanda ilikuwa na historia ya kipekee ya kukaribisha na kusaidia maelfu ya wakimbizi kutoka DRC na Burundi, na akaongezea kwa kusema, nchi hiyo haina uwezo na miundombinu ya kuhudumia wakimbizi kwa kuzingatia mahitaji ya sasa.

Tags