Jul 20, 2022 06:55 UTC
  • Taarifa ya mwisho ya mkutano wa Astana mjini Tehran: Hakuna suluhisho la kijeshi la mzozo wa Syria

Katika taarifa ya mwisho ya kikao cha Astana mjini Tehran, Iran, Russia na Uturuki zimesisitiza kuwa, mzozo wa Syria hauna suluhisho la kijeshi na kueleza azma yao ya kuendeleza ushirikiano wa kupambana na ugaidi wa aina zote.

Mkutano wa saba wa nchi zilizotoa dhamana ya mchakato wa Astana ulifanyika Tehran jana usiku ukihudhuriwa na marais wa Iran, Russia na Uturuki.

Katika taarifa ya pamoja ya marais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Shirikisho la Russia na Jamhuri ya Uturuki, imeelezwa kuwa: Nchi hizo tatu zina dhamira isiyoyumbayumba kuhusu uhuru, kujitawala, umoja na ukamilifu wa ardhi wa Jamhuri ya Kiarabu ya Syria. Pia zimesisitiza malengo na kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kusema kuwa, kanuni hizo zinapaswa kuheshimiwa na watu wote.

Taarifa ya Mkutano huo pia imelaani ongezeko la uwepo na harakati za makundi ya kigaidi na makundi tanzu yenye majina mbalimbali katika maeneo mbalimbali ya Syria, yakiwemo mashambulizi yanayolenga tasisi za kiraia na kusababisha mauaji ya watu wasio na hatia, na kusisitizia haja ya kutekeleza kikamilifu mambo yote yanayohusiana na eneo la kaskazini mwa Syria.

Kuhusiana na suala hili, viongozi wa nchi zilizotoa dhamana ya mchakato wa Astana wamepinga juhudi zozote za kuanzishwa masuala mapya kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, ikiwa ni pamoja na mipango isiyo halali ya kuanzisha mamlaka inayojitawala katika ardhi ya Syria, na wamesisitiza azma yao ya kukabiliana na ajenda za kuanzisha maeneo yaliyojitenga kwa lengo la kudhoofisha mamlaka na ardhi ya nchi hiyo, na vilevile tishio kwa usalama wa kitaifa wa nchi jirani vinavyofanywa kupitia mashambulizi ya kuvuka mpaka na kujipenyeza.

Mkutano wa Tehran

Iran, Russia na Uturuki pia zimeelezea upinzani wao dhidi ya unyakuzi na usafirishaji haramu wa mafuta na mapato ya mauzo yake ambayo ni mali ya Syria.

Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa, viongozi wa nchi hizo tatu kwa mara nyingine wanasisitiza azma yao ya kuendeleza ushirikiano uliopo ili kuangamiza watu wote, makundi, mashirika na taasisi za kigaidi; na wametaka kulindwa raia na miundombinu ya kiraia kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu.

Pande hizo zimeelezea wasiwasi wao mkubwa kuhusu hali ya kibinadamu nchini Syria na vikwazo vyote vya upande mmoja ambavyo ni kinyume na sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na hatua za kibaguzi kupitia utoaji wa misamaha kwa baadhi ya maeneo makhsuusi, jambo ambalo linaweza kusababisha mgawanyiko wa nchi hiyo.

Viongozi wa nchi za Mkutano wa Mchakato wa Amani wa Astana pia wamelaani mashambulizi ya kijeshi yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Syria yakiwemo yale yanayolenga miundombinu ya kiraia na kuyataja mashambulio hayo kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na mamlaka ya kujitawala na ardhi ya Syria na kwamba yanavuruga utulivu na kuzidisha mvutano katika eneo hilo.

Tags