Jaberi Ansari: Madai ya Marekani dhidi ya Iran hayana itibari
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameitaja ripoti iliyotolewa na Marekani ambayo imeiweka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika orodha ya nchi zinazoyaunga mkono makundi ya kigaidi kuwa isiyo na itibari.
Akizungumza katika kikao cha kila wiki kati yake na vyombo vya habari hapa Tehran, Hussein Jaberi Ansari amesema kuwa kwa mtazamo wa Tehran, ripoti ya Marekani dhidi ya Iran haina itibari yoyote na kwamba ripoti hiyo inaweza tu kutajwa kama ripoti ya maelekezo ya kiaidiolijia na yenye kujikariri ambayo Marekani huiwasilisha kila mwaka.
Jaberi Ansari ameongeza kuwa katika ripoti hiyo, Marekani haijaeleza wazi kuhusu uhakika wa mambo ulivyo kwa sababu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yenyewe ni moja ya nchi wahanga wa ugaidi duniani, na katika uwanja huo Iran imepoteza watu elfu 17 kwa ugaidi.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza kuwa, makundi ya kigaidi ambayo hutekeleza oparesheni za kigaidi dhidi ya Iran yanaungwa mkono na nchi za Magharibi khususan Marekani. Jaberi Ansari amesisitiza kuwa Iran hivi sasa iko mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ugaidi na makundi ya kitakfiri huku iikifuatilia suala hili kieneo na kimataifa.