Marandi: Wakati umefika Biden afanye maamuzi magumu
Mshauri wa timu ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia ya Vienna amesema kuwa, wakati umefika kwa utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani kuchukua maamuzi magumu juu ya kuhuishwa makubaliano yanayotarajiwa kufikiwa kuhusiana na kuondolewa vikwazo Iran.
Mohammad Marandi amesema hayo katika ujumbe wake aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, "Iran imetoa jibu lake kama ilivyoahidi, ni wakati wa timu ya Biden kufanya maamuzi ya dhati."
Ameeleza bayana kuwa, kwa Marekani, msamiati wa 'makubaliano ya maana' unamaanisha kukubali masharti ya Washington, lakini kwa Iran, unamaanisha makubaliano ya wastani na yaliyolindwa.
Marandi ambaye pia mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Tehran amebainisha kuwa, iwapo Marekani itafanya maamuzi sahihi, basi makubaliano yatafikiwa haraka iwezekanavyo.
Hapo awali alisisitiza kuwa, Iran inapenda kufikia mwafaka na Marekani, lakini Wamarekani wanapaswa watoe fursa kadhaa pia za upendeleo kwa sababu haiwezekani wao watake kila kitu na wasiwe tayari kutoa chochote.
Kauli ya Marandi imekuja baada ya Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kusema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu usiku wa kuamkia leo Ijumaa imekabidhi mitazamo yake kuhusu majibu ya Marekani juu ya muswada wa makubaliano yanayotarajiwa kufikiwa kuhusiana na kuondolewa vikwazo Iran.
Nasser Kan'ani amesisitiza kuwa, mitazamo hiyo ya Tehran ni ya maana, ya kimsingi na yenye lengo la kufikisha mwisho mazungumzo hayo.