Sep 05, 2022 11:12 UTC
  • Iran: Tuko tayari kuitatulia Ulaya matatizo yake ya nishati

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu imehifadhi hisa yake katika soko la nishati licha ya vikwazo, lakini inaweza kuwa na mchango mkubwa katika kupatia suluhu mgogoro wa niashati unaolikabili bara Ulaya.

Nasser Kanaani amesema hayo leo katika kikao cha kila wiki na waandishi wa habari hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, Tehran iko tayari kuitatulia Ulaya matatizo yake ya nishati, iwapo makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yatahuishwa.

Amesema moja ya malengo makuu ya serikali na taifa la Iran, ni kuondolewa kikamilifu vikwazo haramu wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amekariri kusema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imekabidhi mitazamo yake kuhusu majibu ya Marekani juu ya muswada wa makubaliano yanayotarajiwa kufikiwa kuhusiana na kuondolewa vikwazo Iran na kusisitiza kuwa, Tehran inasubiri majibu ya Marekani.

Mgogoro wa nishati UK

Nchi za Ulaya, ambazo ziliamua kuiwekea Russia vikwazo vya kila aina ili kuishinikiza katika vita vya Ukraine, hivi sasa zinakabiliwa na mgogoro mkubwa wa nishati.

Kadhalika Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kwa mara nyingine ameukosoa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kwa mienendo yake ya siasa. Amesisitiza kuwa, "kuiweka IAEA mbali na siasa ni suala muhimu la dhamana."

Tags