Oct 07, 2022 10:57 UTC
  • Onyo la Iran kwa Umoja wa Ulaya

Hossein Amir Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Jumatano alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Josep Borrell, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya.

Amir Abdollahian alisema kuhusu matukio ya karibuni hapa nchini kwamba: "Sisi tunafuatilia kwa umakini suala la kifo cha Bi Mahsa Amini kwa mujibu wa sheria zetu za ndani ili kujua undani wa suala hilo. Tunayachukulia matakwa ya amani ya wananchi kuwa ni haki yao ya msingi na kuyatilia maanani wakati wote, lakini pamoja na hayo tutakabiliana vilivyo na wafanya ghasia na magaidi kwa mujibu wa sheria za nchi."

Amir Abdollahian ameonya kwamba iwapo Umoja wa Ulaya utachukua hatua za kisiasa na za pupa kwa msingi wa tuhuma ambazo hazijathibitishwa na kwa lengo la kuwachochea wafanya ghasia na magaidi ambao wanalenga roho na mali za watu wa Iran, bila shaka serikali ya Tehran itatoa jibu kali na muwafaka mkabala wa hatua hizo.

Borrell amesema katika mazungumzo hayo ya simu kwamba anakubali kwamba ghasia na ugaidi ni masuala tofauti na maandamano ya amani ambayo yanapaswa kupatiwa majibu yanayofaa. Amesema Ulaya haina nia ya kusababisha matatizo katika mahusiano yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Amir Abdollahian

Licha ya msimamo huo, lakini Josep Borrell siku ya Alhamisi alitoa kauli mpya ambayo ni tofauti na msimamo wake wa hapo awali. Afisa huyo wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya alisema kuwa umoja huo unapanga kutekeleza vikwazo vipya dhidi ya Iran kwa kisingizio cha kile alikitaja kuwa "kukandamizwa na kukamatwa waandamanaji". Alisema Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya watajadili kuiwekea Iran vikwazo zaidi katika mkutano wao ujao. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Catherine Colonna alisema Jumanne kuwa nchi yake inafuatilia kupitia Umoja wa Ulaya suala la baadhi ya maafisa wa Iran kufungiwa mali zao na kuwekewa marufuku ya kusafiri katika nchi wanachama.

Inaonekana Umoja wa Ulaya umeamua kucheza katika uwanja wa Washington kuhusu namna ya kukabiliana na machafuko na ghasia za hivi karibuni nchini Iran, ghasia ambazo zinaungwa mkono kikamilifu na Marekani na utawala haramu wa Israel. Kama unavyofanya kuhusiana na Russia, Umoja wa Ulaya unachukua misimamo ya upande mmoja dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, likiwemo suala la kuiwekea vikwazo vipya ili kuiridhisha Marekani, badala ya kuzingatia maslahi yake yenyewe.

Jambo la kushangaza ni kwamba, Jumatatu Oktoba 3, Rais Joe Biden wa Marekani pia, katika taarifa yake ya kuunga mkono machafuko ya hivi karibuni nchini Iran, alisema kuwa nchi hiyo itawawekea vikwazo vipya maafisa wa Iran, ambao inadai walihusika katika "ukandamizaji wa waandamanaji". Hivyo Ulaya pia inapanga kufuata mfano huo wa Marekan kwa kutishia kuiwekea Iran  vikwazo vipya, bila kutambua kwamba katika miongo michache iliyopita, chombo cha vikwazo kimetumiwa mara nyingi na nchi za Magharibi dhidi ya Iran lakini bila mafanikio yoyote kwa hivyo kimepoteza kabisa itibari yake.

Wakati huo huo, uamuzi wa Ulaya wa kuifuata kibubusa Marekani kwa hakika utakuwa na matokeo mabaya sana kwa Umoja wa Ulaya. Ali Bagheri, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia Masuala ya Kisiasa anasema: "Licha ya kuwa na mikataba ya muda mrefu na mashirika ya Iran na kwa sababu tu ya mashinikizo ya Marekani, nchi za Ulaya zimeamua kuzingatia zaidi maslahi ya Marekani kuliko maslahi yao zenyewe. Ni wazi kuwa hatua hiyo itapelekea kupunguzwa pakubwa uhusiano wa kiuchumi wa Ulaya na Iran na hivyo kudhuru maslahi ya kiuchumi ya nchi hizo. Bila shaka Iran haitakaa kimya mbele ya hatua hizo za uhasama na itachukua hatua zinazofaa kwa ajili ya kulinda maslahi yake ya kitaifa."

Uharibifu uliofanywa hivi karibuni na wahuni na wafanyaghasia mjini Tehran

Inaonekana kwamba onyo kali la Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kwa Umoja wa Ulaya kuhusiana na hatua yake hasi dhidi ya Iran, ikiwa ni pamoja na kuwekewa vikwazo vikali, linaashiria uwezekano wa kuharibika pakubwa uhusiano wa Tehran na Brussels ikiwa nchi za Ulaya zitaendelea kushirikiana na Marekani katika kutekeleza siasa za uchochezi nchini Iran. Iwapo watu wa Ulaya wanataka kweli kuboresha uhusiano wao na Tehran, wanapasa kuachana na siasa za kuifuata kibubusa Marekani na kuwa na uhusiano chanya na Iran kwa msingi wa kuzingatia maslahi ya pande zote mbili.

Tags