Kukiri Marekani kuwa inahusika katika kuchochea ghasia na machafuko nchini Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i89280-kukiri_marekani_kuwa_inahusika_katika_kuchochea_ghasia_na_machafuko_nchini_iran
Ned Price, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, amekiri kwamba utawala wa Joe Biden sasa umejikita kwenye machafuko na ghasia nchini Iran huku akiiishutumu Tehran kuwa haiko tayari kufikia muafaka kuhusu kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Mbali na kukiri huko, imekuwa ikifahamika wazi kimataifa kuwa Marekani inaingilia masuala ya ndani ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 15, 2022 00:10 UTC
  • Kukiri Marekani kuwa inahusika katika kuchochea ghasia na machafuko nchini Iran

Ned Price, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, amekiri kwamba utawala wa Joe Biden sasa umejikita kwenye machafuko na ghasia nchini Iran huku akiiishutumu Tehran kuwa haiko tayari kufikia muafaka kuhusu kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Mbali na kukiri huko, imekuwa ikifahamika wazi kimataifa kuwa Marekani inaingilia masuala ya ndani ya Iran.

Price ametangaza kuunga mkono fujo na ghasia nchini Iran na kusisitiza kuwa lengo la Marekani sasa ni kuwaunga mkono na kuwasaidia wale wanaoibua fujo hizo na kuvuruga usalama wa umma.

Afisa huyo mwandamizi wa Marekani, bila kuashiria matakwa ya kujitakia makuu ya Washington, amedai kuwa matakwa ya Iran hayatekelezeki na ni zaidi ya mapatano ya JCPOA.

Kadhalika, utawala wa Joe Biden, katika mkakati wake mpya wa usalama wa taifa uliochapishwa Jumatano, ulirudia madai kuhusu mpango wa amani wa nyuklia wa Iran na kutangaza hivi: "Tutafuatilia diplomasia ili kuhakikisha kwamba Iran haiwezi kamwe kupata silaha ya nyuklia." Kwa kurudia sera iliyofeli ya "machaguo yote yako mezani", utawala wa Biden, katika muendelezo wa vitisho na diplomasia pamoja na shinikizo lake, umedai kuwa uko tayari kutumia zana zingine ikiwa diplomasia itashindwa."

Marekani, kwa kufichua nia yake ya kweli, yaani kutojali makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kuituhumu Tehran kuwa haiko tayari kwa makubaliano, inaona kuwa, kipindi cha sasa ambacho kina maana ya kutokea baadhi ya machafuko nchini Iran, ni fursa nzuri ya kuingilia mambo ya ndani  ya Iran na kujaribu kudhoofisha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.

Ned Price

Marekani, inadai kuwahurumia wananchi wa Iran na kujaribu kuibua kile kinachodaiwa kuwa eti ni uwazi nchini Iran kwa kufuta vikwazo vinavyohusiana na intaneti. Lakini kinyume cha madai hayo, kilicho wazi ni kuwa Marekani  ni adui mkubwa wa taifa la Iran na mara kwa mara imekuwa ikionyesha uadui wake mkubwa kwa wananchi wa Iran.

Mfano wa wazi wa uhasama huo ni utekelezaji wa kampeni ya mashinikizo ya juu kabisa wakati wa urais wa Donald Trump mwaka 2018. Kampeni hiyo ya uhasama dhidi ya Iran ingali inaendelezwa na rais wa sasa wa Marekani Joe Biden. Mfano wa hivi punde wa uhasama huo ni kuwekewa vikwazo vipya sekta ya usafiri wa anga wa Iran. Vikwazo hivyo vinawalenga moja kwa moja wananchi wa Iran na usalama wa usafiri wa anga.

Mohammad Mohammadi Bakhsh, Mkuu wa Shirika la Usafiri wa Anga la Iran anasema: Licha ya kuzungumza na nchi za Magharibi, Marekani na Ulaya, si tu kuwa hazijachukua hatua yoyote chanya katika sekta ya usafiri wa anga ya abiria bali sasa wameweka vikwazo vipya kwa sekta ya mafuta, ndege na vipuri." Vikwazo hivyo vinaonyesha mtazamo halisi wa nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani kuhusu Iran. Huu ni mtazamo ambao msingi wake ni uadui shadidi dhidi ya taifa la Iran.

Kwa upande mwingine, Marekani inaamini kuwa kwa kutoa vitisho dhidi ya Iran kama inavyoakisiwa rasmi katika hati mpya ya stratijia ya usalama wa taifa ya Marekani, itaweza kuilazimisha Tehran ikubali matakwa yake yasiyo ya kimantiki na haramu katika kadhia ya nyuklia, makombora na sera za kieneo za Iran.

Kuhusiana na hilo, tovuti ya habari ya Hill iliyo karibu na Bunge la Marekani, Congress,  imedai hivi karibuni kwamba wakati umefika kwa nchi za Magharibi kuondoka kwenye meza ya mazungumzo, kutangaza rasmi kuangamia mapatano ya  JCPOA, na kwa utaratibu huo kuanzisha vikwazo na uhasama shadidi zaidi dhidi ya Iran.

Hii ni katika hali ambayo, wanasiasa na wataalamu wa Marekani na duniani kote wamekiri mara kwa mara kushindwa kwa kampeni ya mashinikizo ya juu dhidi ya Iran.

Seneta wa Marekani Chris Murphy anasema: Nukta chanya pekee ya sera mbovu ya "mashinikizo ya juu" ya Trump dhidi ya Iran ni kwamba ilithibitisha kwa hakika kwamba vikwazo vya upande mmoja vinaifanya hali kuwa mbaya zaidi na si bora zaidi. Baada ya sisi kujitoa katika JCPOA, Iran imeimarika zaidi.

Wakati huo huo, kinyume na madai ya Marekani, kufikia makubaliano ya mwisho katika mazungumzo ya Vienna kunasubiri maamuzi ya kisiasa ya Marekani kuhusu masuala kadhaa yaliyosalia. Iran imesema mara kwa mara kwamba ikiwa upande wa Marekani utachukua hatua kwa kuzingatia uhalisia wa mambo, inawezekana kufikia makubaliano. Kati ya matakwa makuu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo ya Vienna ni kupata hakikisho kuwa vikwazo  vitaondolewa na ipate dhamana kuhusiana na uthabiti wa JCPOA na kuondolewa madai ya Wakala wa Umoja wa Mataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA. Aidha Iran inasema itarejea katika mapatano ya JCPOA iwapo tu taifa la Iran litadhaminiwa  faida za kiuchumi.