Dec 04, 2022 09:45 UTC
  • Wanachama wa mtandao wenye uhusiano na Mossad wanyongwa nchini Iran

Wanachama wa mtandao wa majambazi na makundi yenye uhusiano na shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel wamenyongwa alfajiri ya leo nchini Iran.

Vyombo vya habari rasmi vimesema kuwa watu hao wanne walikuwa sehemu ya mtandao wa kijasusi ambao ulikuwa ukishirikiana na shirika ya ujasusi la Israel, Mossad.

Taarifa ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu imesema, kundi hilo lilikuwa lipokea maagizo kutoka kwa maafisa wa Mossad juu ya jinsi ya kutumia bunduki za kivita kwa madhumuni ya utekaji nyara, wizi, kuharibu mali za binafsi na za umma, na kuwalazimisha watu kukiri makosa ambayo hawajayafanya. 

Kwa mujibu wa shirika la habari la Meezan, kutokana na yaliyomo katika failii la kesi hiyo, wahalifu hao walikuwa na historia ya ujambazi, na wahusika wakuu wa genge hilo wamekuwa wakivuruga usalama wa nchi kwa kupokea amri kutoka kwa watu walioko nje ya nchi, na vilevile walikuwa wakipokea fedha kwa ajili ya kvuruga amani nchini. 

Washtakiwa wengine watatu wamehukumiwa kifungo cha miaka 5 hadi 10 jela kutokana na makosa ya jinai kama vile kufanya uhalifu dhidi ya usalama wa nchi, kushiriki katika utekaji nyara na kumiliki silaha kinyume cha sheria.

Hukumu ya kunyongwa vinara wanne wa genge hilo na wahalifu waliokuwa na ushirikiano na shirika la ujasusi la Israel, Mossad, imetekelezwa mapema leo Jumapili. 

Tags