Iran yaitaka Marekani ichukue hatua zaidi kutekeleza mapatano ya nyuklia
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema Marekani inapaswa kuchukua hatua zaidi katika utekelezwaji wa mapatano ya nyuklia kwa kuziruhusu benki kufanya biashara na Iran baada ya kuondolewa vikwazo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema Iran bado haijafaidika na mapatano ya nyuklia ya mwezi Julai baina ya Tehran na madola sita makubwa duniani.
Akiwa katika kikao na waandishi habari mjini Oslo, Norway Jumanne akiwa ameandamana na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini, Zarif ameongeza kuwa: "Naamini Marekani imeondoa vikwazo vyote kwenye makaratasi tu."
Iran inailaumu Marekani kwa kukiuka mapatano ya nyuklia kwa kutoa vitisho kwa benki za dunia ambazo zina hamu ya kufanyabiashara na Iran. Kwa msingi huo benki nyingi, kwa kuhofiwa kuadhibiwa na Marekani, zimejizuia kufanya biashara na Iran.
Zarif amesema utekelezwaji wa mapatano ya nyuklia unapaswa kuwa na faida kwa pande zote.
Kwa upande wake Mogherini amesema Umoja wa Ulaya unahimiza benki na wafanyabiashara wa Ulaya kufanya biashara na Iran. Ameongeza kuwa katika miezi minne ya kwanza mwaka huu, biashara ya Iran na Umoja wa Ulaya imeongezeka kwa asilimia 22.
Ikumbukwe kuwa Iran na kundi la nchi za 5+1 ambazo ni Russia, China, Ufaransa, Uingereza, Marekani na Ujerumani zilitiliana saini mapatano ya nyuklia Julai 14, 2015 baada ya miaka miwili na nusu ya mazungumzo ya kina ya nyuklia.
Kwa mujibu wa mapatano hayo yaliyoanza kutekelezwa Januari 16 mwaka huu, vikwazo vyote vilivyohusiana na miradi ya nyuklia vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya, Marekani na Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran vilipaswa kuondolewa.
Mkabala wa hilo Iran ilitakiwa kupunguza baadhi ya shuguhuli zake za nyuklia. Iran imeshatekeleza ahadi zake lakini nchi za Ulaya na Marekani bado hazijatekeleza ahadi zilizotoa.