Wairani walalamikia ujumbe wa Twitter wa rais wa FIFA
Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Soka Duniani (FIFA) amekosolewa vikali na watumizi wa mitandao ya kijamii wa Iran kwa kutumia neno bandia wakati wa kutaja Ghuba ya Uajemi.
Shirikisho la Soka la Iran pia nalo limelalamikia vikali hatua hiyo ya Rais wa FIFA ya kutumia istilahi isiyo na msingi kuhusu eneo linalojulikana kama Ghuba ya Uajemi wakati akituma ujumbe kuhusu mashindano ya soka ya nchi za Kiarabu.
Shirikisho la Soka la Iran limetoa taarifa na kusisitia kuhusu maana ya Ghuba ya Uajemi huku likiwasilisha malamiko yake rasmi na ya taifa la Iran kuhusiana na kadhia hiyo.
Katika taarifa hiyo, Shirikisho la Soka la Iran limesema litaitumia FIFA nyaraka za kihistoria kuhusiana na Ghuba ya Uajemi ili kusahihisha kosa hilo na kuhakikisha kuwa halikaririwi tena.
Hatua ya Rais wa FIFA Giovanni Vincenzo Infantino ya kutumia neno bandia la 'Kombe la Ghuba ya Kiarabu' badala ya neno sahihi ambalo ni Ghuba ya Uajemi ni jambo ambalo limewakasirisha sana wananchi wa Iran na wengi wamebainisha malalamiko yao kwa kuandika 'Ghuba ya Uajemi' katika ukurusa wa Twitter wa FIFA.