Kan'ani: SEPAH imesambaratisha mikakati ya kibeberu ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i93300-kan'ani_sepah_imesambaratisha_mikakati_ya_kibeberu_ya_marekani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) limesambaratisha njama za maadui hasa Marekani katika ukanda huu na kuufedhehesha utawala wa Kizayuni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 26, 2023 00:32 UTC
  • Kan'ani: SEPAH imesambaratisha mikakati ya kibeberu ya Marekani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) limesambaratisha njama za maadui hasa Marekani katika ukanda huu na kuufedhehesha utawala wa Kizayuni.

Nasser Kan'ani Chafi alisema hayo jana (Jumatano) na huku akiashiria hatua za kiuadui za Marekani dhidi ya wananchi wa Iran amesema kuwa, hatua hizo ni ushahidi wa jinsi maadui walivyohamakishwa na mafanikio ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH).

Amesema hayo kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, vitendo vya kiuadui vya dola la kiistikbari la Marekani pamoja na hatua tofauti na za pande mbalimbali za dhulma na usaliti za tawala za kiimla dhidi ya wananchi wa Iran, ni ushahidi kamili wa kuonesha uongo wa madai ya kisiasa ya kupigania haki za binadamu yanayotolewa na viongozi wa Washington na vibaraka wake.

Wanajeshi vamizi wa Marekani wakiwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislau SEPAH

Amesema, kupanga njama za mapinduzi, kuunga mkono kwa pande zote uvamizi wa serikali ya zamani ya Iraq dhidi ya Iran na kulibebesha taifa la Iran vita vya miaka minane vya kulazimishwa, kuitungua kwa makusudi ndege ya abiria ya Iran, kuendesha vita mseto dhidi ya Iran na kuunga mkono magenge ya kigaidi ni sehemu ndogo tu ya hatua nyingi za kiuadui za dola la kibeberu la Marekani dhidi ya wananchi wa Iran.

Katika kikao chake cha Jumatatu wiki hii, Baraza la Masuala ya Kigeni la Umoja wa Ulaya liliamua kuliweka jina la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) katika orodha ya kile kinachodaiwa eti ni makundi ya kigaidi.