Feb 09, 2023 10:48 UTC
  • Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu asisitiza ulazima wa kuwepo umoja wa kitaifa na kukabiliana na mikakati ya adui

Umoja wa kitaifa na umoja wa jamii una nafasi maalum kwa watu wa kila nchi. Bila kuwepo umoja wa kitaifa, uhai wa nchi na taifa hauwezi kupatikana. Umoja wa kitaifa unamaanisha umoja wa taifa kubwa na lenye fahari la Iran ambao ni siri ya ushindi wa taifa hili na sababu ya kuimarishwa jamii.

Walengwa hapa ni raia wa taifa, maafisa wa mfumo na mashirika ya serikali. Kwa msingi huu, Imam Khomeini-Mwenyezi Mungu Amrehemu- alilitilia maanani suala hili la kimsingi na aliamuru umoja wa kitaifa ndani ya nchi na katika umma kwa ujumla, na hali kadhalika alisisitiza kuimarishwa umoja wa Kiislamu baina ya mataifa ya Kiislamu.

Mshikamano wa Kiislamu maana yake ni huruma, usuhuba na udugu wa Waislamu duniani kwa misingi ya Uislamu na tauhidi, na hiyo ndiyo amri iliyo wazi ya Mwenyezi Mungu, Mwenye hekima, na viongozi Maasumu, Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yao.

Waislamu wanatakiwa na Qur'ani Tukufu kuwa ni wenye umoja. Hivyo umoja wa Kiislamu ni siri kuu na ufunguo wa kutatua matatizo yote ya Waislamu. Kwa hakika umoja unawafanya Waislamu wajihisi kuwa wenye nguvu.

Kwa hiyo, Uislamu unawaamrisha Waislamu kuwa wamoja na kuepuka mifarakano. Qur’ani inauzingatia umoja na mshikamano huu kwa kuwataka Waislamu wafungamane na Kamba ya Mwenyezi Mungu na wasifarakiane sambamba na kumfuata Mtume Muhammad SAW. Aidha Kwa msingi huo kupuuza amri za Mwenyezi Mungu na Mtume wake  ni sababu ya mgawanyiko na mfarakano wa jamii.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran pia yalipata ushindi katika kivuli cha umoja na mshikamano wa wananchi wa Iran chini ya uongozi wa Imam Khomeini-Mwenyezi Mungu Amrehemu. Kwa kuasisiwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, maadui wa kieneo na kimataifa wakiongozwa na Marekani, hawajajizuia kuchukua hatua ya kuidhoofisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati wowote ule, na katika mwelekeo huu, sasa kuliko wakati mwingine wowote, wanataka kuleta migawanyiko na mifarakano katika jamii na watu wa Iran na kujenga mazingira ya kutoaminiana baina ya makundi mbalimbali ya watu, viongozi wa mfumo unaotawala wa Kiislamu na wafuasi wa madhehebu ya Kiislamu.

Imam Khomeini-Mwenyezi Mungu Amrehemu

Katika hotuba zake, Imam Khomeini alilitaka taifa la Iran mara kwa mara kudumisha umoja na mshikamano kwa sababu aliuona umoja wa taifa zima kuwa ndio ufunguo wa ushindi. Kwa maneno mengine umoja wa kitaifa ndio uliopelekea kupatikana ushindi mkubwa wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Imam Khomeini, katika sehemu ya wasia wake wa kisiasa, anasema kuhusu siri ya ushindi na siri ya kubakia Mapinduzi ya Kiislamu: Bila shaka, siri ya kubakia Mapinduzi ya Kiislamu ni siri ile ile ya ushindi, na taifa linajua siri ya ushindi na vizazi vijavyo vitaikumbuka katika historia na siri hii ina nguzo kuu mbili ambazo ni msukumo wa Mwenyezi Mungu na kufikiwa lengo kuu la kuasisi serikali ya Kiislamu pamoja na kujumuika taifa lote nchini katika umoja wa neno kwa ajili ya kutimiza msukumo na lengo hilo hilo.

Suala hili ambalo maana yake ni ulazima wa kuwepo umoja wa kitaifa na kuepusha mifarakano na pia kutilia maanani stratijia ya adui katika uga wa kuibua hitilafu na kuweka pengo baina ya wananchi, limekuwa likitajwa mara kwa mara na Ayatullah Khamenei,  Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Kuhusiana na suala hilo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu siku ya Jumatano, katika kikao na makamanda na wafanyakazi wa Kikosi cha Anga na Kikosi cha Ulinzi wa Anga katika Jeshi la Iran, kwa mara nyingine tena aliashiria suala hilo muhimu na lenye kuainisha hatima. Ayatullah Khamenei amesema katika muktadha huu kwamba: Moja ya mahitaji yetu muhimu zaidi leo ni umoja wa kitaifa. Umoja wa kitaifa ni ngao na ngome imara dhidi ya adui. Mshikamano na umoja wa kitaifa ni nukta ambayo ilikuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya ushindi wa mapinduzi na kisha katika ustawi wa Mapinduzi. Leo tunahitaji kuongeza umoja huu kadri tunavyoweza.

Wakati huo huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mara nyingine tena ametahadharisha kuhusu stratijia ya adui ya kuzusha hali ya kutoaminiana na hitilafu katika jamii ya Iran na kusema: "Mbinu za adui ni kuzusha hali ya kutoaminiana. Kutokuwa na imani kunapotokea, tumaini la mustakabali pia hutoweka. Kutokuaminiana kunaweza kuwa ni kati ya makundi ya kisiasa, kutokuaminiana makundi ya wananchi, wananchi kutoaimini serikali, serikali kutowaamini wananchi na kutokuaminiana mashirika ya kiserikali. Hitilafu huwa zinaibuka lakini tofauti hizi zisigeuzwe kuwa ufa. Wakati mwingine maadui huibua masuala ya wanawake, wakati fulani wanaleta malumbano ya Shia na Sunni,  wakati mwingine masuala mbalimbali na wakati mwingine wanaibua tofauti baina ya vizazi ili kuleta hitilafu na migawanyiko.

Tags