Feb 12, 2023 12:09 UTC
  • Juhudi tasa za miongo minne za Marekani za kuuangusha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Mamilioni ya Wairani jana Jumamosi walishiriki katika maandamano ya maadhimisho ya tarehe 22 Bahman (Februari 11) na kuadhimisha kwa hamasa kubwa miaka 44 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Wananchi wa Iran walishiriki katika maadhimisho hayo na kusisitiza mshikamano wao mkubwa, kizazi baada ya kizazi, na thamani za Mapinduzi ya Kiislamu, wakipeperusha bendera ya Uislamu na kuzidisha matumaini ya kupata ushindi watu wote wanaokandamizwa na kudhulumiwa katika maeneo mbalimbali duniani.

Sherehe za mwaka huu za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran zilikuwa na ladha ya kipekee, hasa baada ya kufeli njama kubwa iliyoanzishwa na madola ya kigeni dhidi ya Iran ya Kiislamu katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, iliyolenga usalama wa ndani na umoja na mshikamano wa taifa kwa kuibua ghasia na kuziunga mkono kupitia vita mseto vya kisiasa, kiuchumi na hujuma ya vyombo vya habari vya Magharibi. Hata hivyo hujuma na vita hivyo vilishindwa kutokana na mwamko, umakini, kusimama kidete, umoja na mshikamano wa wananchi na hekima ya viongozi wao.

Akihutubia hadhara kubwa ya wananchi katika mzunguko wa Azadi jiji la Tehran, Rais Ebrahim Raisi alisema kuhusiana na mafanikio yaliyopatikana nchini katika nyuga mbalimbali za sayansi, teknolojia, uchumi, ulinzi, afya na tiba kwamba adui hawezi kuyavumilia maendeleo na hatua ilizopiga Iran.

Aidha alisisitiza kuwa, licha ya vitisho na vikwazo mbalimbali, leo hii Iran ya Kiislamu imefanikiwa katika vigezo vya ukuaji thabiti wa mitaji, ukuaji wa kiwango cha uwekezaji, ukuaji wa uchumi na ukuaji wa vigezo vingine.

 

Jamhuri yaKiislamu ya Iran imeandhimisha mwaka wa 44 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yaliyopata ushindi 1979 kwa uongozi wa Imam Ruhullah Khomeini katika hali ambayo, wanasiasa wa Marekani wamewahi kutoa matamshi ya vitisho na majigambo na kudai kwamba, mapinduzi haya hayawezi kufikisha miaka 40. John Bolton ambaye amewahi kushika nyadhifa muhimu nchini Marekani ukiwemo wadhifa wa mshauri wa usalama wa taifa, aliwahi kudai kwamba, kabla ya mapinduzi haya kufikisha umri wa miaka 40, kundi la kigaidi la munafiqin litakuwa likitawala nchini Iran.

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, daima Marekani imekuwa na utendaji wa kihasama na kiuadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kufanya njama kila uchao kwa ajili ya kuuondoa madarakani mfumo wa Kiislamu unaotawala hapa nchini. Sambamba na hayo, katika kipindi cha miongo minne iliyopita, Marekani imetelekeza siasa za kuishinikiza na kuiwekea vikwazo Iran. Katika kipindi cha uongozi wa Rais Donald Trump vikwazo vya upande mmoja vya Marekani vilifikia katika hatua ya kiwango cha juu kabisa na ambacho hakijawahi kushuhudiwa.

 

Hata hivyo pamoja na njama zote hizo, Marekani imeshindwa kufikia malengo yake haramu. Baada ya kuibuka maaandamano miezi michache iliyopita hapa nchini kwa kisingizio cha kifo cha Mahsa Amini, Marekani na waitifaki wake waliona hiyo kama fursa nyingine muhimu ya kuitumia kwa ajili ya kuushinikiza mfumo wa Kiislamu na pengine hata kuuondoa madarakani. Ni kwa msingi huo, ndio maana viongozi wa Marekani na washirika wao walijitokeza na kuwaunga mkono waziwazi wafanya fujo na machafuko hapa nchini ambapo wachache waliohadaiwa na maadui walikuwa wakiharibu mali za umma na za watu binafsi.

Msimamo thabiti wa serikali, uungaji mkono wa wananchi na sera za kimuqawama za Iran zimeweza kusambaratisha njama zote za maadui na jana Iran imeadhimisha miaka 44 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu tena kwa mahudhuruio makubwa na kuwatangazia maadui kwamba, mfumo wa Kiislamu nchini Iran ungali una uungaji mkono mkubwa wa wananchi wenye ghera na nchi hiyo.

Tags